Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAFANYABIASHARA, wakulima na wananchi kwa ujumla wanaohusika na uchakataji wa bidhaa wameshauriwa kuzalisha bidhaa zinazozingatia usalama na ubora ili kulinda afya na usalama wa mtumiaji.
Ushauri huo ulitolewa na Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka, wakati akitoa elimu kwa washiriki na wananchi wa Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya Nanenane mkoani Dodoma. Maonesho hayo yameanza Agosti 1 hadi 8, mwaka huu.
Mwabuka, alisema shirika hilo limetoa elimu hiyo kwa wafanyabiashara, wakulima na wananchi waliojitokeza kwenye maonesho hayo ili waweze kufahamu kwamba bidhaa wanazochakata sio kwa ajili ya Mkoa wa Dodoma peke yake, bali ni kwa ajili ya nchini nzima na soko la nje ya nchi, hivyo lazima ziwe na alama ya ubora.
"Soko la Dodoma sio la kwenu peke yenu, ni soko la Kimataifa, ni SADC (Jumuiya ya Nchi Kusini mwa Afrika) ni Soko la Afrika Mashariki (EAC) na ni soko la dunia, hivyo kama bidhaa zenu hazikidhi ubora maana yake hazitakubalika sokoni," alifafanua Mwabuka na kusisitiza;
Aidha, aliwaambia washiriki wa maonesho hayo na wananchi kwa ujumla kwamba kilimo ni biashara, hivyo kuanzia kwenye mchakato wa kilimo hadi mwisho ni lazima bidhaa iwe na ubora na salama ili inapopelekwa sokoni, ipokelewe na wananchi na mwisho wa siku ishindane kwenye soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, Mwabuka alisema TBS inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure, kwani gharama zote zinalipwa na Serikali, hivyo wanachotakiwa ni kuwa na barua ya utambulisho kutoka SIDO.
Kwa mwaka Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya sh. milioni 150 hadi 200 kwa ajili ya kuthibitisha bidhaa zao bure.
"Kwa hiyo waitumie TBS ili kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa salama, kwani gharama zao zinalipwa na Serikali," alisisitiza.
Aidha, aliwataka wananchi kuhakikisha bidhaa wanazotumia zina salama ya ubora ili ziwe salama kwa matumizi.