Ruangwa - Lindi
Imeelezwa kuwa, Serikali inaandaa Mkakati wa kuwezesha uongezaji thamani madini kwa lengo la kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini utakaopelekea Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua rasmi Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayokwenda sanjari na Kongamano la Wadau wa Madini ya Chumvi Mkoani Lindi leo Agosti 21, 2023
"Serikali inaendelea kuhimiza uongezaji thamani madini nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini. Katika kuhakikisha kuwa kusudio hilo linafikiwa, nawaomba wawekezaji kuendelea kuwekeza katika viwanda vya uongezaji thamani madini," amesema Dkt. Kiruswa
Aidha amesema, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini ili kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi, amesema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Sera mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji, Viwanda na Biashara nchini.
"Ninapenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wadau wote wakiwemo washirika wetu wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi, napenda pia kuwashukuru washiriki wote mliotoka sehemu mbalimbali mliojumuika na wananchi wa Mkoa wa Lindi hii leo, hakika uwepo wenu unadhihirisha umuhimu wa maonesho haya kwamba sio tu kwa watu wa Lindi bali ni dhamira ya Serikali yetu ambayo ina nia kubwa ya kuendelea kuona Mkoa wa Lindi na Mikoa mingine ya Ukanda huu wa Kusini inafunguliwa kiuchumi," amesema Dkt. Kiruswa
Vile vile, Serikali itaendeleza jitihada za kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na ujenzi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainabu Telack amesema kuwa kupitia maonesho haya wawekezaji wanajionea fursa mbalimbali za rasilimali madini ikiwa pamoja na kutangaza fursa nyingine za kiuchumi zinazopatikana mkoani Lindi.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ni *"Wekeza Lindi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Maendeleo ya Jamii"*. Maonesho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini waliopo ndani na nje ya nchi yanayoendelea hadi Agosti 26 mkoani Lindi.