Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imekamilisha Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme kilichopo Ifakara (Ifakara Substation) na kuleta neema ya umeme wa uhakika kwa wananchi wa wilaya za Kilombero na Ulanga mkoani Morogoro, ambao walikuwa na changamoto ya kupata umeme mdogo na wenye kukatika mara kwa mara.
Kukamilika kwa Mradi wa ujenzi wa Kituo hicho chenye uwezo wa MVA 20 wa Msongo wa Kilovoti 220, kumetokana na mikakati mahsusi ya Serikali kupitia REA, inayolenga kuhakikisha wananchi wote wakiwemo waishio vijijini wanapatiwa umeme wa uhakika.
Akizungumza usiku wa Agosti 28 mwaka huu, wakati wa kuhitimisha zoezi la kuunga Kituo hicho kwenye Gridi ya Taifa, Meneja wa Mradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena alieleza kuwa azma ya kutekeleza Mradi huo ilifikiwa baada ya Wakala kubaini changamoto ya umeme mdogo waliyokuwa wakiipata wananchi wa maeneo hayo na hivyo kudhamiria kuitatua.
Mhandisi Lwena alisema, changamoto hiyo ya umeme mdogo imesababisha hali ya uwekezaji katika wilaya hizo kuwa chini pamoja na uwezo mzuri unaotokana na uwepo wa bidhaa za kilimo katika eneo hilo.
“Kwa hivyo, kukamilika kwa Mradi huu, kutawezesha sasa kufungua fursa za uwekezaji kutokana na kuwepo umeme wa uhakika. Pia, kutatatua changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara na zaidi, wananchi sasa wataweza kufanya kazi za ujasiriamali za aina mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi na kujiongezea kipato,” alisema Mhandisi Lwena.
Aidha, manufaa mengine yanayotokana na kukamilika kwa Mradi huu ni kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweza kupeleka umeme wa Gridi katika maeneo mengine yaliyo jirani ikiwemo Ulanga. Hii ni kufuatia REA kukamilisha kazi yake ya kujenga Mradi na kuukabidhi kwa TANESCO ambayo ndiyo huhusika na usimamizi na uendeshaji wa miundombinu yote ya umeme nchini.
Mradi wa Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara, ulikuwa na mafungu mawili, moja likiwa ni ujenzi wa Kituo hicho na jingine linahusisha usambazaji wa nishati ya umeme kwa wananchi ambayo yote yamekamilika na kubaki kazi ndogo ya kukamilisha kuhakiki vifaa vilivyoungwa ili kuhakikisha viko sawa tayari kwa kuanza kutumika.
Mradi umegharimu jumla ya Euro Milioni 8.75 ambazo ni takribani shilingi bilioni 22 za Tanzania ambapo kati yake, Euro Milioni 2.25 ni fedha za Serikali na Euro Milioni 6.5 ni ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya.
Taswira ya Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara. Kituo hiki kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika wilaya za Kilombero na Ulanga.
Mafundi wakiwa katika hatua za mwisho kukamilisha kazi ya kujenga Mnara wa kupeleka umeme kwenye Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara ambacho kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya Euro Milioni 8.75 (Shilingi bilioni 22 za Tanzania) zilizotolewa na Serikali ya Tanzania pamoja na ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya.
Meneja wa Mradi wa Kituo cha Kupoza Umeme Ifakara, Mhandisi Dominicus Lwena akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kukamilika kwa kazi ya kuunganisha kituo hicho kwenye Gridi ya Taifa, Agosti 28, 2023. Ujenzi wa Kituo hicho umetekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya Euro Milioni 8.75 (Shilingi bilioni 22 za Tanzania) zilizotolewa na Serikali ya Tanzania pamoja na ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya.