Breaking

Thursday, 31 August 2023

PPRA: Mfumo mpya wa NeST utaongeza fursa kwa Makundi Maalum

Na Mwandishi Wetu , Dodoma

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewasisitizia watu waliopo kwenye makundi maalum ambayo ni vijana, wazee, wanawake na watu wenye ulemavu kujisajili kwenye Mfumo Mpya wa Ununuzi kwa njia ya Mtandao (NeST) ili kunufaika na upendeleo uliopo katika fursa za ugawaji wa Zabuni za umma nchini.

Akizungummza leo kwenye kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Bw. Eliakm Maswi amesema kuwa Mfumo wa NeST unawatambua na kuwazingatia wazabuni waliopo kwenye makundi hayo.

“Mfumo unawatambua watu wa makundi maalumu, kwa hiyo wanachotakiwa kufanya ni kufuata taratibu za kurasmisha vikundi vyao katika ngazi za halmashauri kisha wajisajili kwenye mfumo wa NeST”. Alisema Maswi

Aidha, amesema kuwa Katika Mfumo wa TANePS usajili wa makundi maalumu haukuwa mkubwa, hivyo amewasihi wenye sifa za kuwa makundi maalum na wanahitaji kushiriki zabuni za umma kujisajili katika mfumo wa NeST ambao ni rafiki zaidi kwa watumiaji wote. .

“Serikali yetu inawajali watu wote na inataka kila mtanzania mwenye sifa aweze kushiriki zabuni za umma na kujiinua kiuchumi, sio tu kwa makampuni hata watu binafsi waliosajiliwa pamoja na watu ambao wako katika uchumi wa chini ambao wanaweza kushiriki kupitia fursa ya makundi maalum hata bila kuwa makampuni, alisema.

Alisisitiza kuwa zipo kazi nyingi ambazo kwa mujibu wa sheria zimetengwa kwa ajili ya makundi maalumu na kwamba mfumo wa NeST utaongeza kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wazabuni kwa kuwa unaongeza uwazi, ushindani na kuondoa urasimu usio na sababu za msingi.

Fursa za ugawaji wa zabuni kwa makundi maalumu zinasimamiwa na kushughuliwa kwa kuzingatia vifungu vya Sheria ya ununuzi ya Umma sura 410 inayozitaka taasisi zote za umma nchini kutenga asilimia 30 ya bajeti ya Ununuzi kwa mwaka kwa ajili ya makundi maalumu. Aidha, kwa mujibu wa Mwongozo wa Makundi Maalumu uliotolewa na PPRA mwaka 2020, makundi maalumu yamegawiwa asilimia 10 kwa vijana, asilimia 10 kwa watu wenye ulemavu, asilimia 5 kwa wanawake na asilimia 5 kwa ajili ya wazee.

Bw. Maswi alisema kuwa PPRA bado inaendelea kutoa mafunzo wezeshi ya matumizi ya Mfumo wa NeST kwa Wazabuni na Taasisi nunuzi kote nchini ili kuhakikisha kuwa umma wa watanzania wanajengewa uwezo na kuchangamkia fursa katika ununuzi wa umma nchini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi (wa pili kulia) na Meneja wa Huduma za Mafunzo na Ushauri, Castor Komba (wa kwanza kushoto) akiwasilisha mada katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Agosti 30, 2023 mjini Dodoma

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages