Breaking

Saturday, 26 August 2023

MCHENGERWA – TAMASHA LA KIZIMKAZI NI ZAIDI YA TAMASHA, AFURAHISHWA NA MECHI WA SIMBA NA YANGA


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amesema Tamasha la Kizimkazi linalotarajia kufanyika Zanzibar ni tamasha muhimu linalokufungamanisha utalii na utamaduni ambalo inayowaunganisha wananchi wote bila kujali itikadi za siasa au dini.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo Agosti 25, 2023 kuelekea tamasha la Kizimkazi baada ya kushuhudia mechi ya kirafiki baina ya mashabiki wa Simba na Yanga wanaoishi Makunduchi visiwani Zanzibar.

Mechi hiyo ya kihistoria iliyokusanya maelfu ya wananchi na wapenzi wa soka kutoka katika kila kona ya Tanzania imedhaminiwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) chini ya Mwenyekiti na Mwanzilishi wake Mhe. Wanu Hafidh Ameir.

Hadi mwisho wa mechi hiyo timu zote zilikuwa zimetoka ya sare ya bao 1-1 na baada ya kuelekea kwenye penati timu zilitoka suluhu bila kupata mshindi, hivyo kuamriwa kurudia mechi hiyo Agosti 31mwaka huu.

Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa michezo na utamaduni vikitumika vizuri na kufungamanishwa na utalii vitasaidia kukuza amani, mshikamano lakini pia kuleta mapato na kuimarisha uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Kama ambavyo leo tumeshuhudia wenyewe watanzania kutoka katika kila kona ya nchi yetu wamefika kwenye mechi hii ya watani wa jadi bila kujaliitikadi zao za dini na vyama vya siasa na hiyo ndio inaleta tafsiri ya Tanzania aliyotuachia baba wa Taifa Mwalimu Nyerere”. Ameeleza Mhe. Mchengerwa

Mechi hiyo pia ilipambwa na msanii nguli wa singeli Sholo Mwamba ambaye alikonga nyoyo za mashabiki wa Simba na Yanga.

Aidha amesema matamasha ya aina ya Kizimkazi yanasaidia kurithisha hazina ya utamaduni ambao unazaa utamaduni wa utalii utakaosaidia kujenga msingi wa utalii endelevu.

Ameongeza kuwa kwa sasa nchi nyingi duniani zinajivunia utalii wao ambapo amefafanua kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na tamaduni nzuri ambazo ni kivutio kikubwa kwa wageni kuja kujionea.

Amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj.Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuifungua Tanzania duniani kupitia Filamu ya The Royal Tour ambapo kwa sasa amesema imesaidia kuteta wimbi kubwa la watalii na kutoa wito kwa wananchi kuwekeza katika miundombinu kama vile nyumba za kulala wageni wanapokuwa nchini.

Aidha, amesema amani na utulivu uliopo ndiyo nguzo na kivutio kikubwa kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kutembea na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwa ni pamoja na tamaduni za watanzania.

Tamasha la mwaka huu ya Kizimkazi limeboreshwa zaidi ambapo wadau mbalimbali wameshiriki ikiwa ni pamoja na Wanyama mbalimbali kama simba chui na pundamilia wanaoneshwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages