Breaking

Sunday, 20 August 2023

MARYPRISCA AWATAKA WANUFAIKA WA MRADI WA MAJI MSHIKAMANO KUWA NA SUBIRA

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka wananchi hususani wa Kata ya Mbezi, Ubungo na Mshikamano ambao ni wanufaika wa mradi wa maji Mshikamano kuwa na subira ya kuwaunganisha na huduma kwa kuwa kazi ya ufundi huwa inatekelezwa kwa kuzingatia utaratibu.

Ameeleza hayo wakati wa ziara yake ya siku ya pili alipotembelea utekelezaji wa mradi wa maji Mshikamano uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Amesema kuwa mradi huu wa Mshikamano umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na DAWASA na ni mradi ambao utajibu shida ya maji kwa wananchi wengi wa maeneo haya.

"Tumesikia shuhuda nyingi kutoka kwa wananchi kuwa maeneo haya yalikuwa makame kwa mrefu, lakini kwa jitihada kubwa za DAWASA maeneo mengi yameanza kupata maji, tunaishukuru DAWASA kwa namna ambavyo wanaiwakilisha vizuri Wizara ya Maji," ameongeza Mhandisi Maryprisca.

"Wito wangu kwa wananchi ambao wameshalipia maunganisho ya maji wawe na subira kwa kuwa kazi za kiufundi zinakwera kwa utaratibu, tayari vifaa vya maunganisho mapya vimeshanunuliwa na wateja mtaanza kuunganishiwa hivi karibuni," Mhandisi Marryprisca Mahundi Naibu Waziri wa Maji.

Mhandisi Maryprisca amefafanua kuwa utoaji wa kumbukumbu namba za wananchi walioomba maji ulisimama kwa muda ili kufuatilia upatikanaji wa vifaa vya maunganisho ya maji, na kwa sasa vifaa vimepatikana hivyo wananchi watapewa namba na kuunganishiwa na huduma.

Tunampongeza sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake wa kutoa fedha za mfuko wa Uviko kiasi cha bilioni 2.5 kwenye mradi wa maendeleo ili wananchi wapate maji.

Nae Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Shaban Mkwanywe amesema anaishukuru Serikali kupitia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kutekeleza mradi huu na kuukamilisha.

Mradi huu unatuwezesha kujibu hoja za shida ya maji kwa wananchi, kwa sasa kazi tunayoendelea nayo ni kusambaza maji kwa wananchi kwa kasi.

"Kwa mwaka huu wa fedha 2023/24 tumetenga fedha za ndani bilioni 2.5 kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi wote wa kata ya Mbezi, Msakuzi kusini na kaskazini kuwa wasiwe na wasiwasi huduma itafika," ameeleza Mhandisi Mkwanywe.

Mkazi wa Kata ya Mshikamano Ndugu Sanga Mbowe ameishukuru Serikali kupitia DAWASA na kuomba kazi ya kusambaza maji ifanyike kwa haraka ili wananchi wote waweze kunufaika na huduma.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages