Breaking

Wednesday, 16 August 2023

MABORESHO HUDUMA YA MAJI YALETA UNAFUU WA MAISHA KINONDONI



Na Mwandishi Wetu

Kamati ya siasa ya Wilaya ya Kinondoni imeeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi ya Majisafi ikiwemo utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo ulioleta unafuu wa maisha kwa wakazi takribani 12,000.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Ndugu Shaweji Mkumburwa wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji wa Makongo hadi Bagamoyo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia ufadhili wa benki ya Dunia na ulitekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilion 71.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeleta ahueni ya maisha ya wananchi wengi wa Wilaya ya Kinondoni ikiwemo maeneo ya *Madale, Wazo, Mivumoni, Goba, Mbweni, Tegeta* na maeneo jirani ambao awali hawakuwa na huduma ya maji hivyo kuwalazimu kununua kwa gharama kubwa.

“Hapa lazima tuwe wakweli, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imeboresha maisha ya watanzania wengi na wakazi wa Kinondoni wakiwemo. Tunajivunia hili na tunasema hapa Mamlaka yetu ya DAWASA imeweza kutekeleza hili kwa weledi sana” alisisitiza.

"Sisi kama kamati ya Siasa ya Wilaya tunapenda kuwatoa wasiwasi baadhi ya Wananchi wa maeneo ambao bado hawajaunganishiwa huduma, kuwa kazi bado inaendelea kufanywa na wenzetu DAWASA kupitia utekelezaji wa mradi huu mkubwa hivyo kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji." amesema Ndugu Mkumburwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amesema kuwa wananchi wanapaswa kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha maji yanapatikana kwa kila mwananchi, na kutoa wito kwa Wananchi wachache kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ya maji kwa kuwa serikali inatumia gharama kubwa kwenye miradi hii.

Naye, Meneja wa DAWASA Mivumoni, Ndugu Gilbert Massawe amesema kuwa hadi sasa mradi umekamilika na kazi iliyobaki ni kufanya maunganisho madogo madogoili kuwafikia wananchi wote ili waweze kupata huduma ya maji.

"Mamlaka inahakikisha vifaa vinapatikana kwa wakati na kazi ya maunganisho kwa wananchi inaendelea kufanyika kwa haraka ili kila mwananchi apate huduma ya maji," ameeleza Ndugu Massawe.

Utekelezaji wa Mradi wa usambazaji maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo unanufaisha kunufaisha wakazi zaidi ya 450,000 ulitekelezwa kwa lengo la kuondoa changamoto ya huduma ya maji na kuhusisha ujenzi wa matanki matatu ya kuhifadhi maji katika maeneo ya Vikawe, Mbweni na Tegeta A pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages