Breaking

Friday, 18 August 2023

DAWASA YAWANOA MABALOZI WA USAFI WA MAZINGIRA MASHULENI




Klabu za maji na usafi wa Mazingira za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kutoka shule za Sekondari Zanaki na Kibasila zimepata mafunzo ya huduma za usafi wa mazingira kwa lengo la kuwajengea Wanafunzi uelewa wa utunzaji wa miundombinu ya majitaka kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa huduma za Usafi wa Mazingira DAWASA, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema kuwa mafunzo hayo ni mahususi ili kuwapa ujuzi wa matumizi bora ya miundombinu ya majitaka , kufahamu hatua mbalimbali za uchakataji majitaka pamoja na madhara ya uharibifu wa mifumo hiyo pindi inapoharibiwa.

Mkurugenzi Lydia pia alitoa rai kwa wanafunzi hao kujikita katika masomo ya sayansi na kujifunza fani ya uhandisi wa Majitaka kwani kuna bado idadi ndogo ya wataalamu katika fani hiyo huku uhitaji ukiwa ni mkubwa.

"Fani ya usafi wa Mazingira hasa Majitaka ni nzuri na bado ina wataalamu wachache, hivyo katika masomo yenu mzingatie masomo na kwa wale watakaopenda wajifunze masuala ya majitaka basi wachangamkie zaidi masomo ya sayansi”. amesema Mhandisi Ndibalema.


Pia amesisitiza matumizi bora ya vyoo kwa kutotupa taka ngumu kama plastiki, nguo chakavu, taulo za kike katika miundombinu ya majitaka na kuwasihi wanafunzi kuwa mabalozi wazuri katika jamii zao ili kuboresha hali ya usafi wa mazingira.

Kwa upande wake mwalimu wa shule ya sekondari Kibasila , mwalimu Emmanuel Sedekia ameishukuru DAWASA kwa kuanzisha klabu za mazingira mashuleni zinazosaidia kuwajengea wanafunzi utamaduni wa utunzaji wa mazingira na kupitia klabu hizi watapatikana mabalozi na viongozi bora siku za usoni.

“Hii ni hatua ya mfano ambayo DAWASA imeitekeleza, na klabu hizi zitatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa katika kuhakikisha utu na mazingira unapewa kipaumbele”. ameeleza Mwalimu Sedekia.

Mwanafunzi Isaac Heshton kutoka klabu ya maji na usafi wa mazingira Shule ya Sekondari Kibasila, ameishukuru DAWASA kwa kuwa ziara ya mafunzo kujifunza katika usimamizi wa utoaji huduma bora ya majisafi na usafi wa Mazingira.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages