Breaking

Friday, 11 August 2023

DAWASA YAAINISHA MIKAKATI USAMBAZAJI MAJI 2023/24



Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam [DAWASA] imeainisha mikakati mbalimbali ya kuboresha upatikanaji wa maji kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo jumla ya bilioni 425.9 zimetengwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya majisafi na usafi wa mazingira kwenye eneo kihuduma.

Utekelezaji wa miradi hii imelenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote kufikia asilimia 95 mwaka 2025.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2023/24 jijini Dodoma, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa mikakati hii inaenda sambamba na malengo endelevu ya maendeleo hasa lengo namba 6, dira ya Taifa inayotutaka tuwe tumefikisha majisafi kwa asilimia 95 ya wakazi tunaowahudumia.

“Ni katika muktadha huu ndipo tunapokwenda kubuni miradi ya kimkakati na kuitekeleza kufikia malengo yetu, malengo ya serikali na kuchangia katika kukidhi makubaliano ya kimataifa,’’ amesema Ndugu Kiula.

Amebainisha kuwa katika kufanikisha malengo haya, Mamlaka imeanza utekelezaji wa miradi mikubwa 8 ya kipaumbele ikiwemo mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji, mradi wa maji Kwala, mradi wa maji Pangani Kibaha, mradi wa Kimbiji mpaka chuo cha uhasibu, mradi wa kusini mwa Dar es Salaam, mradi wa uchimbaji visima 9 vya Kimbiji, mradi wa usafi wa mazingira ya kuboresha afya na mazingira, mradi wa kukabiliana na upotevu wa maji kwa kutumia mifumo ya teknolojia ambayo yote inatekelezwa kwenye eneo la kihuduma.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia DAWASA inatekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kwa lengo la kuhakikisha kuwa maji katika mto Ruvu yanakuwepo mwaka mzima. Amesema mpaka sasa Mkandarasi anaendelea na kazi kwa kasi ili kuweza kumaliza ndani ya miaka mitatu kwa mujibu wa mkataba.

"Nipende kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa ushirikiano mkubwa wanaotupa katika kuboresha upatikanaji wa huduma katika maeneo tunayohudumia," ameeleza Ndugu Kingu.

Mbali na hayo, Ndugu Kingu ameeleza mafanikio ya kazi ya usambazaji maji kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/23, ambapo jumla ya miradi ya kimkakati 7 iliyogharimu bilioni 219 pamoja na miradi midogo midogo 86 ya kusogeza huduma kwa wananchi ilitekelezwa.

Amebainisha kuwa miradi iliyotekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Zegereni, Soga na Mbwawa Pwani, mradi wa maji Kigamboni, Mshikamano, miradi ya majisafi nje ya mtandao, mradi wa maji Bagamoyo hadi Chuo kikuu, mradi wa lipa kwa matokeo, mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu na mradi wa maji Makabe.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages