Breaking

Thursday, 27 July 2023

WAZIRI MKUU WA BURUNDI ATEMBELEA MAKAO MAKUU TPA NA BANDARI YA DAR ES SALAAM.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya BURUNDI Mhe. GERVAIS NDIRAKOBUCA amesema bandari ya Dar es Salaam imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu NDIRAKOBUCA amesema hayo tarehe 27 Julai,2023 mara baada ya kutembelea bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza utendaji kazi wake.

“ Tunafurahishwa sana na kazi hii inafanyika hapa Bandarini, tunaona jitihada kubwa inayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Shehena yetu ya Burundi inafika ikipitia katika Bandari hii na kusaidia sana katika kukuza uchumi wa Nchi yetu. Tunaishukuru sana Serikali yenu na tunaomba MUNGU aendelee kuimarisha ushirikiano mwema kati ya Burundi na Tanzania.” Amesema Waziri Mkuu Ndirakobuca

Aidha Waziri Mkuu Ndirakobuca ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha ulinzi katika mipaka ya Tanzania na Burundi na hivyo kuleta utulivu, kupunguza uharifu na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika.

Awali wakitoa maelezo kuhusu utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi PROF.MAKAME MBARAWA na Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa wamemuhakikishia Waziri Mkuu huyo kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPA, inaendelea kufanya maboresho makubwa katika bandari zake ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam huku ikiendelea kufungua milango kwa Sekta Binafsi kushiriki katika kuendesha na kuendeleza Bandari na hivyo kuendelea kuchochea uchumi wa Tanzania na Burundi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages