NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WANAVITUO vya Taarifa na Maarifa vya Mkoa wa Dar es Salaam vinavyosimamiwa na Shirika la Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP, wamefanya ziara ya kutembelea Kituo cha Kilimo Malolo cha Mabwepande kilicho chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwaajili kujifunza masuala ya ujasiriamali kupitia Kilimo na Ufugaji.
Akizungumza leo Julai 14,2023 kwenye ziara hiyo, Mwanachama wa TGNP, Bi.Rehema Mwateba amesema ziara hiyo inalenga kuinua mbinu za ujasiriamali biashara kwa washiriki ili vituo vyao vya Taarifa na Maarifa viweze kuwa na mfuko imara wa fedha kwaajili ya kuwezesha shughuli za harakati kwenye kata zao.
Amesema kupitia ziara hiyo wanavituo vya taarifa na maarifa wanakwenda kushirikiana kujadili hali ya ukosefu wa usawa wa kijinsia na nini kifanyike kupitia ujasiriamali na biashara.
Aidha, Bi. Mwateba amesema wanavituo vya taarifa na maarifa wanakwenda kuimarika kwa harakati za kusaidia jamii kutambua mapungufu ya kijinsia tunayoishi nayo.
"Haya mafunzo tunayoyapata ni kwaajili ya kuimarisha uelewa wa masuala ya jinsia, ujasiriamali na biashara kwa wanavituo vitano vya taarifa na maarifa". Amesema Bi.Mwateba.
Kwa upande wa washiriki kwenye ziara hiyo wamewapongeza TGNP kwa kufanikisha ziara hiyo kwani wameweza kujifunza mambo mengi yanayohusu kilimo cha biashara pamoja na ufugaji ambapo wanakwenda kuimarika na kuyafanyia kazi yale yote ambayo wamejifunza katika vituo vyao.