Na Mwandishi Wetu
SHULE ya Sekondari Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam imeendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita ambapo mwaka huu wanafunzi 38 wamepata daraja la kwanza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Mkuu wa shule hiyo, Emil Rugambwa, alisema kwenye matokeo hayo wanafunzi wake wengine 62 wamefaulu kwa daraja la pili wakati wanafunzi 15 pekee wamepata daraja la tatu.
Rugambwa aliwapongeza wanafunzi kwa matokeo mazuri na kuahidi kuwa shule hiyo itaendelea kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya.
Alisema matokeo hayo mazuri ni matunda ya jitihada kubwa inayofanywa na walimu na menejimenti ya shule hiyo katika kuwaandaa wanafunzi kwenye mtihani ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya.
“Nawashukuru walimu wangu kwa jitihada kubwa wanazofanya kufundisha wanafunzi na kufanikiwa kupata matokeo haya na kama kawaida yetu hatujapata daraja la nne wala 0 hili ni jambo la kujivunia,’ amesema
Baadhi ya wazazi waliozungumzia matokeo hayo ya Tusiime walisema wamefurahishwa na matokeo ya shule hiyo kwani wanafunzi wengi wamepata ufaulu wa juu.
Mmoja wa wazazi hao ambaye mtoto wake amefanya vziuri kwenye shule hiyo, Aisha Bakari, alisema wameyapokea matokeo hayo kwa furaha kubwa kwasababu ufaulu umekuwa mkubwa na hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la tatu wala 0.
"Walimu wa Tusiime wanafundisha kwa kweli maana matokeo haya yamekuwa mazuri sana na tunawaomba walimu waendelee na moyo huu huu wa kufundisha na wafanye vizuri zaidi na zaidi,” alisema
Mzazi mwingine Mwita Wandwi, alipongeza shule hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya mwaka hadi mwaka.
"Tusiime imekuwa ikifanya vizuri na kwa kweli wanaendelea kufanya vizuri nimeangalia matokeo ya mwaka huu kidato cha sita mtoto wangu amepata daraja la kwanza na point nne naona kwangu ni fahari kubwa sana na wengine wamepata ufaulu wa juu sana wanastahili pongezi,” alisema
Mzazi Samson Chale, alizungumza kwa simu alisema matokeo yamewafurahisha sana na kwamba bila shaka ni matunda ya jitihada za walimu na uongozi wa shule hiyo ambao wamekuwa bega kwa bega na wazazi wa wanafunzi katika kufuatilia maendeleo ya taaluma ya wanafunzi hao.
“Nakumbuka kwenye shindano la mdahalo wa kielimu lililoshirikisha nchi mbalimbali barani Afrika miaka ya karibuni wanafunzi wa Tusiime waliibuka na medali nane na shindano hilo lilifanyika Dar es Salaam Tusiime walipata tuzo ya mzungumzaji bora kwa upande wa wavulana, mzungumzaji bora chipukizi, mzungumzaji bora wa jumla kwenye shindano hilo na mzunguzaji bora wa kike,” alisema.
Alisema medali hizo ziliiweka shule ya Tusiime kwenye nafasi ya pili kwenye mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 38.
Mkurugenzi wa Shule za Tusiime, Albert Katagira, aliipongeza bodi ya shule hiyo wazazi, walimu, wafanyakazi wote wa shule na wanafunzi kwani mafanikio hayo yametokana na mchango wao mkubwa.
Mkurugenzi wa shule za Tusiime za Tabata Dar es Salaam, ambazo zimeendelea kufanya vziuri kitaaluma, Albert Katagira kushoto akiwa na Mkuu wa shule ya Sekondari Tusiime, Emil Rugambwa kulia.
Mkuu wa shule ya sekondari Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam, Emil Rugambwa, akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano wa shule hiyo kuhusu matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa juzi na Baraza la Taifa la Mitiha ni NECTA ambapo wanafunzi 38 wa shule hiyo wamepata dalaja la kwanza na wengine 62 kupata daraja la pili.