Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewataka Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu nchini.
Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kuhusu Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) utakaosaidia kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu nchini.
Amefafanua kuwa, kama Tume ya Utumishi wa Walimu itafanya kazi yake ipasavyo, itaweza kuirahisishia kazi Ofisi ya Rais -TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kushughulikia changamoto mbalimbali za Walimu nchini.
Amesema Walimu ni nguzo muhimu katika taifa, hivyo wanatakiwa kupewa huduma stahiki ili waendelee kuondoa changamoto ya ujinga katika jamii bila kukumbana na changamoto yoyote.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mhe.Simbachawene amewataka watumishi wa Tume hiyo kutenda haki kwa kuwasikiliza na kutoa matumaini kwa Walimu kutokana na changamoto wanazokumbana nazo ili waweze kufurahia utumishi wao.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzifanyia kazi changamoto za Walimu na kusisitiza kuwa Rais Samia anataka ifikapo Agosti mwakani, changamoto za Walimu ziwe zimeisha kabisa akitolea mfano changamoto ya malimbikizo ya mishahara na kupanda madaraja.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi amesema idadi kubwa ya wateja wanaofika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni Walimu na kwamba hiyo ni ishara kuwa changamoto zao hazifanyiwi kazi kikamilifu katika Tume ya Utumishi wa Walimu.
Amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumushi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu wataendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu hao ili waweze kufanya kazi kwa ari kubwa.