Breaking

Saturday, 22 July 2023

TOENI ELIMU VIJIJI VINAVYOPANDISHWA HADHI-DKT MABULA

Na Munir Shemweta, WANMM BIHARAMULO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka ofisi za ardhi kuhakikisha zinafuata taratibu na kutoa elimu kwa wananchi hasa katika ardhi za serikali za vijiji zinapopandishwa hadhi na kuwa mamlaka za miji.

Waziri Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 21 Julai 2023 katika eneo la Lusahunga wilayani Biharamulo mkoani Kagera alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Rulenge na serikali ya kijiji cha Lusahunga.

Mgogoro huo umeibuka kufuatia serikali ya kijiji cha Lusahunga kutaka sehemu ya eneo lililoombwa na Kanisa Katoliki kwa madai kuwa ndiyo yenye mamlaka. Hata hivyo, Tangazo la Serikali Na 76 la mwaka 1996 lilitangaza eneo hilo kuwa mamlaka ya mji na kulifanya kutoka katika sheria namba 5 ya vijiji na kwenda sheria ya mipango miji.

Sheria namba 8 ya mipango miji ya mwaka 2007 inaipa mamlaka halmamshauri ya wilaya kusimamia mpango wa uendelezaji na hivyo kufanya serikali ya kijiji kutokuwa na mamlaka tena ya kugawa ardhi.

‘’Maeneo ya vijiji yanapopanda hadhi ni lazima taarifa zifike kwa wahusika ili wajue kuwa sasa eneo hili haliko kwetu na liko kwenye mamlaka nyingine’’ alisema Dkt Mabula

Alisema, wilaya ya Biharamulo ina vijiji vingi vilivyopandishwa hadhi na katika kuepuka migogoro ya aina hiyo ameelekeza halmashauri ya wilaya kupita kijiji kwa kijiji kufahamisha wananchi mabadiliko hayo.

‘’Ninaelekeza mkawafahamishe kwa maandishi viongozi wa serikali za vijiji vilivyopandishwa hadhi kuwa hawaruhusiwi kugawa ardhi tena na kama watahitaji kwa ajili ya shughuli za kijiji basi watawasiliana na ofisi ya mkurugenzi kwa kuwa mamlaka ya usimamizi wa utawala wa ardhi hayako kwao tena yapo halmashauri ya wilaya’’ alisema Dkt Mabula

Alisema, watumishi wa sekta ya ardhi wakifuata taratibu sambamba na kuwafahamisha wananchi mabadiliko yanayotokea kwa vijiji vinavyopandishwa hadhi basi hakutakuwa na migogoro na wakati huo shughuli katika maeneo hayo zitakuwa zimewezeshwa.

‘’Eneo lako likipimwa na kupata hati unaweza kuitumia kuchukulia mkopo benki kwa kuwa ardhi yako itakuwa imepanda thamani na hata unapotaka kuuza ni tofauti na yule asiye na hati’’. Alisema Dkt Mabula

Akigeukia mgogoro kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya kijiji cha Lusahanga, Dkt Mabula ametaka makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili ya Kanisa Katoliki kupatiwa ekari 50 yaendelee na kusimamiwa na mkuu wa wilaya na kueleza kuwa ekari 95 zilizobaki zitakuwa chini ya halmashauri ya wilaya ya Biharamulo ambapo kama kijiji kikitaka eneo kinapaswa kuomba huko.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa tatu kushoto) akifuatilia maelezo ya Mkuu wa wilaya ya Biharamulo Advera Bulimba wakati alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo la Lusahunga Wilayani Biharamulo mkoa wa Kagera tarehe 21 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Biharamulo Advera Bulimba wakifuatilia maelezo yanayotolewa na Razalo Kasigala kuhusina na mgogoro wa ardhi baina ya Kanisa Katoliki na serikali ya kijiji cha Lusahunga tarehe 21 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kulia) akimsikiliza Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara Severine Niwemugizi alipowenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Kanisa Katoliki na serikali ya kijiji cha Lusahunga tarehe 21 Julai 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Lusahunga wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera alipowenda kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Kanisa Katoliki na serikali ya kijiji cha Lusahunga tarehe 21 Julai 2023.
Sehemu ya wananchi wa Lusahunga wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya Kanisa Katoliki na serikali ya kijiji cha Lusahunga tarehe 21 Julai 2023.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages