Nchi za Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha utafiti wa kilimo na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima wa Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Mjini Jeonju-si,Korea Kusini wakati wa mazungumzo ya ushirikiano baina ya Naibu Waziri wa Kilimo wa Tanzania Mh. Anthony Mavunde na Ndg. Yun Jongchul Makamu Mtawala Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na Utafiti ya Korea(Korea Patnership for Innovation in Agriculture- KOPIA).
Kupitia mazungumzo hayo Naibu Waziri Mavunde ameiomba KOPIA kuanzisha kituo chake nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) ili kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika tafiti za kilimo kwa lengo la kumsaidia mkulima kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia kanuni bora za kilimo,uzalishaji mbegu bora na teknolojia ya kisasa ya kilimo,sambamba na hayo Naibu Waziri Mavunde ameomba pia ushirikiano wa kitaalamu katika utekelezaji wa Programu ya Vijana ya Building a Better Tomorrow-BBT.
Naye Ndg. Yun Jongchu*l Makamu Mtawala Mkuu wa KOPIA ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na utashi wa kukuza sekta ya kilimo na kuongeza bajeti ya kilimo kwa kiwango kikubwa,na kuahidi kwamba Korea Kusini kupitia KOPIA wapo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika uanzishwaji wa kituo cha KOPIA TANZANIA ili kusaidia katika kukuza utafiti wa kilimo na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kilimo hasa katika Programu ya BBT.
Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini,Balozi Togolan Mavura ameishukuru Taasisi ya KOPIA kwa utayari wao kufanya kazi na Tanzania na kuahidi kusimamia makubaliano hayo ya uanzishwaji wa kituo cha KOPIA TANZANIA ambacho kitakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya kilimo nchini Tanzania katika kutekeleza Ajenda 10/30.