NA MWANDISHI WETU
Mbunge wa Kuteuliwa Riziki Lulida amesema kuwa Sekta ya Madini imezidi kuwatetea na kuwainua watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kuwapa nafasi katika kushiriki shughuli mbalimbali za uzalishaji kupitia Shirika la Madini nchini (STAMICO).
Lulida ameyasema hayo July 10, 2023 alipotembelea Banda la Wizara ya Madini, katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Maarufu Sabasaba ambapo amesema kuwa serikali imeendelea kuyatambu, kuyapa kipaumbele na kuyawezesha makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi.
“Ndani ya Sheria ya Umoja wa Mataifa iliwekwa kabisa Sheria ya mwaka 2007 kuwa haki za walemavu zinashirikishwa, lakini katika sheria hii niipongeze STAMICO kwa juhudi kubwa inayofanya kwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki ndani ya taasisi yao, katika taasisi hii ya STAMICO imeweza kutenga machimbo ya madini kwa watu wenye ulemavu wa kusikia ambao ni viziwi, lakini vilevile STAMICO limeshirikisha taasisi ya watu wenye ulamavu wa ngozi,” amesema Lulida
Lulida amesema STAMICO limekuja na kauli mbiu ya ‘Tupa shoka panda mti’ kwaajili ya kusaidia watu wenye ulemavu na tayari Shirika hilo limewasaidia watu hao kwa kuwapatia miti na kuwasaidia katika upandaji wa miti hiyo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, lakini pia ameyaomba Mashirika mengine kuiga mfano wa STAMICO katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.
“Nimezunguka katika mabanda mengi, lakini kufika hapa nimeona nisiwe mchoyo wa kusema ukweli kuwa STAMICO inafanya kazi,” na kuongeza kwa kuwaomba vijana wasio na ulemavu kuchangamkia fursa hususani katika shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kuendelea kulalamika kwamba hakuna ajira.
Kwa upande wake Kelvin Nyema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania, ambaye pia ni Msimamizi wa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu Viziwi kutoka Mkoani Geita amewaomba watu, mashirika na taasisi mbalimbali kuwasaidia kwa kuwawezesha katika shughuli za uzalishaji uchumi.
“Uchimbaji wa dhahabu unategemea mambo mengi hasa katika ubebaji wa mawe ya dhahabu, STAMICO wametusaidia mafunzo ya usalama katika uchimbaji wa dhahabu pamoja na biashara ya dhahabu tayari wametupa vifaa mbalimbali mfano kofia, viatu, mavazi mbalimbali, STAMICO wametusaidia sana, Malengo yetu ni kupata dhahabu za kutosha,” amefafanua Nyema.
Kwa upande mwingine Said Kabembe Mkurugenzi Mtendaji wa Mwamvuli wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Watu Wenye Ulemavu Tanzania amesema misaada wanayopata katika shughuli za uchimbaji madini kwenye migodi mbalimbali imeleta mabadiliko katika maisha kwa kuwafanya kuchapa kazi, badala ya kuendelea kusubiri kuomba omba mtaani.
“Watu wenye ulemavu huwa tunaamini siku zote tukiwezeshwa tunaweza STAMICO wamekuwa miongoni mwa mashirika ambayo yanatufanya tuweze kupitia kutuwezesha, kwahiyo niwaombe wasituchoke, lakini pia mashirika mengine, wadau mbalimbali waige mfano wa STAMICO ili watu wenye ulemavu tusitofautiane sana na wale walioko Ulaya.” Ameeleza Kabembe.
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Maarufu Sabasaba yanaendelea katika Viwanja vya Sabasaba yalianza June 28 2023 na yanatarajiwa kutamatika July 13, mwaka huu.