Breaking

Thursday, 13 July 2023

SHIRIKA LA POSTA KINARA TUZO SABASABA



Shirika la Posta Tanzania limeibuka kinara katika tuzo za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), zilizotolewa leo tarehe 13 Julai, 2023, katika viwanja vya Maonesho Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zilizoratibiwa na TANTRADE, zimekabidhiwa na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi katika kufunga Maonesho hayo.


Aidha, Shirika la Posta limekuwa mshindi wa Kwanza katika kundi la Mtoa huduma bora za Usafirishaji (Courier and Logistic Exhibitor) wa mwaka katika maonesho hayo. Kwa sasa Shirika limeendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji nchini hususani katika kuongeza magari yake na pikipiki kwa ajili ya usambazaji wa mwisho (last mile delivery) na matumizi ya TEHAMA katika usambazaji.



Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Bw. Amos Millinga ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, ameishukuru TANTRADE kwa kutambua mchango wa Posta hasa katika shughuli za Usafirishaji, kwani tuzo hizo zitaendelea kuchochea na kuongeza hamasa kwa Shirika kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Meneja wa Banda la Shirika la Posta Tanzania Bw. Khamis Swedi ametumia nafasi hiyo kushukuru wananchi, wadau pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Posta kwa kuliunga mkono Shirika wakati wa kipindi chote cha maonesho hadi kufikia ushindi huo.

Maonesho haya yaliyokuwa na Kauli Mbiu ya “Tanzania ni Mahali sahihi Pa Biashara na Uwekezaji” yalianza rasmi tarehe 28 Juni, 2023 na yamefungwa leo tarehe 13 Julai, 2023.

TANTRADE ndiye mratibu wa kuandaa tuzo hizi kila mwaka kwa kutambua mchango wa Taasisi/Mashirika/Kampuni katika kutoa huduma kwa wananchi hususani katika kipindi cha maonesho ya Sabasaba.


Imetolewa na;
Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano;
Shirika la Posta Tanzania.
13 Julai, 2023.










Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages