Breaking

Thursday, 6 July 2023

SERIKALI YAPATA MUAROBAINI KUKABILI UVAMIZI WA TEMBO NCHINI


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua programu maalum ya ujenzi wa vituo maalum 16 kwa ajili ya kuthibiti wanyama wahalibifu katika maeneo mbalimbali nchini vitakavyogharimu zaidi ya bilioni moja.

Akizindua program hiyo na kushiriki kwenye ujenzi wa kituo cha kudhibiti Wanyama waharibifu katika Kijiji cha Muheza wilayani Same mkoani Kilimanjaro Julai 5, 2023 amefafanua kuwa program hiyo ni mkakati maalum ambao utasaidia kukabiliana na wimbi la wanyama waharibifu hususan tembo ambao wameongezeka kwa kiasi mkikubwa katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kuimarika kwa uhifadhi.

Amesema Wizara itapeleka Askari wa kutosha wa uhifadhi kwenye kila kituo ambao watatakiwa kushirikiana na wananchi kwenye maeneo husika kuwakabili wanyama hao pindi wanapotokea kwenye makazi ya wananchi na kuwarejesha katika hifadhi.


Amezitaka taasisi zote zilizochini ya wizara yake kuwa na ushirikiano mkubwa na wananchi ambapo amewataka kushuka chini kwa wananchi na kufanya uhifadhi wa raslimali hizo kwa karibu huku akifafanua kuwa wahifadhi namba moja wa raslimali ni wananchi.

Akifafanua kuhusu program hizo amesema program hiyo ni mkakati madhubuti na endelevu wa kuhakikisha kuwa changamoto hiyo inapata ufumbuzi wa kudumu.

Aidha amelielekeza Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) kuhakikisha linaleta helikopita ndani ya siku mbili katika eneo la Same kwa ajili ya kuja kusaidia zoezi la kuondoa makundi ya wanyama Tembo walio kwenye maeneo ya makazi na kuwarejesha Hifadhini. Eneo hili lipo karibu na Hifadhi ya Mkomazi ambayo ina idadi kubwa ya Tembo.




Baadhi ya wakazi wa eneo hili wamepongeza jitihada kubwa inayofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi hiki kupitia ya Maliasili na Utalii ambapo wamesema mikakati hiyo ya itasaidia kupata mazao ambayo yamekuwa yakiliwa na Tembo mara yanapokomaa.

“Nampongeza Rais Samia kwa kutuletea vituo hivi ambavyo ni mkombozi wetu kwa kuwa kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tukishindwa kuvuna mazao yetu kwa sababu ya kuliwa na tembo.” Amefafanua Juma Khalifa Mkaazi wa eneo hilo

Waziri Mchengerwa ametaja maeneo nane ya awali yatakayojengwa vituo hivi kupitia Mamlaka ya Ngorongoro kuwa ni pamoja na Same, Kilosa, Manyoni, Monduli, Korogwe, Babati, Morogoro vijijini na Rufiji

Pia ameiagiza Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kujenga vituo nane kama hivi kwenye maeneo mengine yenye changamoto zaidi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages