Breaking

Wednesday, 5 July 2023

ORYX GASI YAGAWA MITUNGI YA GESI 500 KOROGWE IKIHAMASISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA WENYEVITI, WATENDAJI

Na Mwandishi Wetu, 

KAMPUNI ya Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited imegawa mitungi na majiko yake 500 kwa Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji na Kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku ikieleza lengo la kugawa mitungi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa mitungi hiyo mbele ya viongozi hao wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Araman Benoite amesema wamekuwa wakiendelea kufanya uwekezaji mkubwa nchini Tanzania kwa makundi mbalimbali ya wananchi ili kuunga mkono juhudi za serikali.

"Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya LPG ambayo ni suluhisho la kuondoa matumizi ya kuni na mkaa, hivyo basi kuboresha afya ya jamii na kulinda mazingira,sambamba na ahadi ya Rais kutoa nafasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia."

Aidha amesema katika muendelezo uleule wa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nshati safi ya kupikia kwa wananchi wote,kampuni ya Oryx Gas imeamua kusimama na wananchi wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kupitia kwa viongozi wao kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wote.

"Juhudi hizi ni pamoja na kusaidia kuwabadilisha viongozi wa wananchi kuachana na kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati ya gesi za kupikia (LPG).Hivyo tumekabidhi mitunge ya gesi na majiko 500, " amesema na kuongeza ugawaji huo umekwenda sambamba na kutoa mafunzo ya usalama wa matumizi ya mitungi hiyo.

Benoite amesema wanaamini viongozi wanawakilisha wananchi na kiongozi anapaswa kuongoza kwa mifano na wanaushawishi mkubwa kwa wananchi wanaowaongoza hivyo Oryx imeona itoe mitungi ili wao wenyewe wakianza kutumia watape mamlaka ya kuwaambia wananchi umuhimu wa mabadiliko.

Pia amesema Oryx Gas Tanzania Ltd inaendelea kuwekeza katika uagizaji, uhifadhi, ujazaji wa gesi kwenye mitungi na usambazaji wa LPG Tanzania nzima, pamoja na Visiwa vyake. Oryx Gas Tanzania huwekeza kila mwaka mamilioni kadhaa ya dola kwenye mitungi mipya inayoingizwa sokoni kila siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amesema ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi inakwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye alishazindua kampeni ya kutumia nishati mbadala kwa lengo la kulinda mazingira.

Amesema katika wilaya hiyo wameamua kugawa mitungi hiyo ya gesi kwa viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya mpaka ngazi ya msingi wakiwemo wenyeviti wa vijiji na watendaji katika kata zote huku akifafanua lengo kubwa ni kutoa ujumbe kwamba miti mingi inayokatwa iko vijijini na huko ndiko ambako viongozi hao wapo.

”Wenyeviti na watendaji wa vijiji tumewaona na tumetambua uwepo wenu, kama viongozi kwenye maeneo yeenu kuna watu wanawaakangalia. Leo hii mwenyekiti wa kijiji na mtendaji wake wakiamua kutumia nishati mbadala na wanakijiji watahamasika.

"Kwasababu wanaangalia viongozi wao wanawajua, wamewachagua wenyewe na wana uwezo wa kuwashawishi kuacha kutumia miti vibaya wakaanza sasa kuunga mkono jitihada hizi za kutumia nishati mbadala ili tuokoe kizazi hiki na kinachokuja."

Aidha ameeleza kutokana na uharibifu wa mazingira Serkali ilitoa maelekezo mahususi wananchi kupandeni miti na kutunza mazingira , vyanzo vya maji ili kupata maji lakini kilimo kibaki salama kuwe na chakula cha kutosha.

“Sasa maamuzi ni ya kwetu sisi, na ndio kwenye haya nikasema lazima sisi viongozi katika ngazi zote ndani ya wilaya ya Korogwe tukubaliane tuachane na matumizi ya mkaa na kuni.Tukiamua kubadilika tutachochea wenzetu kubadilika.

“Nikasema sipendi kushurutisha watu bila kuwezesha , majiko ya gesi ndio haya kazi kwenu , lakini hii ni awamu ya awali tumeshauriana na viongozi wenzangu hivyo tutaenda awamu kwa awamu.Nia yangu ni kuwa na Korogwe inayosomeka kama wilaya kinara kwenye matumizi ya nishati safi,”amesema Jocate.

Ameongeza suala la nishati safi ya kupikia ni la wote hivyo watalibeba kwa mikono miwili ili kunusu misitu na mazingira sambamba na kwenda na kauli ya Rais Dk.Samia ya kuigeuza Tanzania salama na yenye kusifika katika utunzaji mazingira na kutumia nishati safi ya kupikia.

“Huo ndio mtazamo wetu na katika kufanikisha tumeungwa mkono na wenzetu wa Oryx ambao wanasifika kwa kugawa mitungi lakini mimi ningependa wasifike kwa watu unaowagawia mitungi waendelee kutumia hii mitungi.Watu lazima waendelee kutumia gesi na hii iwe endelevu,"amefafanua.


Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo(katikati) ,Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Tanzania Araman Benoite (wa pili kulia) pamoja na Meneja Mauzo Ukanda wa Dar es Salaam na Pwani Shaban Mohamed(wa tatu kushoto) wakimkabidhi mtungi wa gesi Rose Kimweri ambaye ni miongoni mwa viongozi na mjasiriamali katika wilaya hiyo.
Sehemu ya watendaji na wenyeviti kutoka kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakiwa makini kufuatilia uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia sambamba na ugawaji wa mitungi ya Oryx Gas kwa viongozi wa ngazi mbalimbali
Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx GasTanzania Araman Benoite akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wenyeviti na watendaji wa Wilaya ya Korogwe kuhusu namna salama ya kuutumia mtungi wa gesi.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo akizungumza wakati wa tukio la ugawaji mitungi 500 iliyotolewa na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa watendaji na Wenyeviti wote wa kata 40 zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga

Meneja Masoko wa kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akitoa maelezo kwa watendaji na wenyeviti katika kata mbalimbali za halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakati akitoa elimu ya usalama wa matumizi ya gesi

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages