Na Said Mwishehe, Kondoa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana, amewahimiza wana CCM kuwa wamoja na kujenga mshikamano ili kwenda katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 pamoja na uchaguzi mkuu wakiwa wamoja na kuibuka washindi pamoja.
Akizungumza leo Julai 23, 2023 kwenye kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kondoa mkoabi Dodoma pamoja na mambo mengine Kinana ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wana CCM kuendelea kuwa wamoja katika kila jambo hasa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani .
"Nipongeze kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa CCM hususan katika ngazi kitongoji, Kijiji, mtaa na Kata kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mwakani ni mwaka wa Uchaguzi, hivyo naamini wana CCM tutakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka 2024 tukiwa kitu kimoja," amesema Mzee Kinana.
Ametumia nafasi hiyo kueleza Chama pia kinatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotelewa na viongozi wa CCM katika ngazi za kata, vitongoji, vijiji, wilaya na mkoa kwani wao ndio wanaokutana na wananchi na wakati wa uchaguzi ndio wanaokwenda kuomba kura.
Pia, amewapongeza madiwani wanaotokana na CCM ambao wamekuwa wakisimamia ngazi ya Kata na wamekuwa wakifanya hivyo bila ya kuwa na mshahara lakini wameendelea kujitoa kwa kuwatumikia wananchi.