Na Johnn Mapepele
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Mkoa wa Pwani na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema wananchi wanatakiwa kulinda amani iliyoletwa na Serikali ya CCM kwa kuwa ndiyo muhimili pekee wa kuwaletea maendeleo.
Akizungumza kwenye Mkutano Maalum wa CCM, Wilaya Kibiti leo mjini hapo ambao Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Komred Abdulrahman Kinana amekuwa Mgeni Rasmi ambapo amesisitiza kuwa Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya kulinda amani katika kipindi cha awamu zote hivyo hawana sababu ya kuhangaika kuchagua viongozi wa vyama vya upinzani.
Aidha, amefafanua kuwa Serikali ya awamu hii chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wake na kwamba maendeleo hayo yamefanyika kila kona ya Tanzania katika kipindi kifupi cha miaka miwili.
Mkutano huo maalum wa Wilaya ya Kibiti ulikuwa na ajenda ya kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 kwa kipindi cha Oktoba 2020 hadi Juni 2023 wa miradi ya Maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 32 katika wilaya hiyo.
Akizungumzia kuhusu jimbo lake la Rufiji, Mhe. Mchengerwa amesema anamshukuru Rais Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha za maendeleo ambazo zimeleta mapinduzi makubwa kwenye sekta zote kuanzia uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, sekta ya elimu, Afya na kilimo.
Amesema mkakati wa sasa ni kuwaleta wawekezaji ili waje kuwekeza katika miradi mbalimbali katika jimbo hilo hususan kwenye eneo la ujenzi wa mahoteli na zoo kwa ajili ya kufugia Wanyama kwa kuzingatia kuwa ukanda huu ni miongoni mwa kanda zenye Wanyama wengi wa porini.
Ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuyatambua maeneo ya uwekezaji na kuwekeza ambapo pia amefafanua kwamba anatarajia kuendelea kufanya onesho kubwa desemba mwaka huu la kumuenzi mwanasiasa Mkongwe hayati Bibi Titi Mohamed ambalo mbali na kuelezea historia ya wanarufiji litatumika kutangaza viovutio na fursa za uwekezaji katika wilaya ya Rufiji.
Makamu Mwenyekiti Komred Kinana amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kama Mbunge na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa mkoa wa Pwani.
Aidha, amesifu kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea watanzania maendeleo katika kipindi kifupi ambapo amefafanua kuwa inatokana na mahusiano mazuri aliyoyajenga na mataifa mbalimbali duniani. Amewaomba watanzania kuiendelea kumwombea
Amesema hii ndiyo awamu pekee ambayo Serikali imepata fedha nyingi za ufadhili na kwamba katika kipindi hiki Serikali imefanya ujenzi mkubwa wa miundombinu ikiwa ni pamoja na madarasa na zahanati.