--Azindua shina la vijana la ushirika Ikwiriri
Na Johnn Mapepele
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amefungua Shina la Ushirika la Umoja wa Vijana wa Ikwiriri wilayani Rufiji na kuwataka kuwapuuza watu wanaopinga uwekezaji unaofanywa na Serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii amesema hayo mara baada ya kuzindua rasmi wa Shina hilo na kupandisha Bendera ya CCM ambapo pia aliwapa kadi za CCM vijana kadhaa waliohama kutoka vyama vya upinzani.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa mpango wa uwekezaji unaofanywa na Serikali katika bandari hiyo unakwenda kuingiza mapato makubwa ambayo yatasaidia kusukuma sekta nyingine ukilinganisha na mapato kidogo yanayopatikana sasa.
Aidha, amewasihi watu wenye hoja za msingi kuziwasilisha serikalini ili zifanyiwe kazi badala ya kuwadanganya wananchi kwa tamaa zao za kutaka kushika dola.
Amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii ili kukuza mapato yao na uchumi wa taifa zima kwa kujumla na kufafanua kuwa hayo yanawezekana endapo vijana hawataruhusu amani ya nchi ichezewe na watu ambao amewaita ni waroho wa madaraka.
“Tusiruhusu watu wachache walipasue taifa hili kwa kusema uongo na kushawishi watu, tunapaswa kuilinda amani hii tuliyoachiwa na baba wa Taifa kwa nguvu zetu zote, uzuri wa Tanzania ni kwa sababu Tanzania ina amani. Tutahakikisha Tanzania inaendelea kuwa moja” amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema hivi karibuni kumekuwa na watu wachache ambao wanatumia ajenda ya kupinga uwekezaji katika bandari ili waweze kushika dola jambo ambalo amesema halikubaliki.
Amewataka kujiunga katika vikundi ili waweze kujirasimisha na kuweza kukopesheka kirahisi na kupata fedha za maendeleo kwa ajili ya kufanyia uwekezaji katika shughuli mbalimbali za biashara.
Aidha amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya maendeleo hivyo hakuna sababu ya watanzania kudanganywa na watu wasiyoitakia mema Tanzania
Tukio la uzinduzi wa shina la CCM lilipambwa na wasanii wa wilaya ya Rufiji ambao walitoa burudani ya kukata na baada ya hapo Mhe. Mchengerwa alipita kuzungumza kupokea kero mbalimbali za wananchi katika viunga vya mji wa Ikwiriri.