Breaking

Saturday, 1 July 2023

MBIO ZA KIMONDO ZAFANA SONGWE

Mashindano ya riadha, maarufu kama Mbio za kimondo yanayoandaliwa kwa pamoja baina ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimondo duniani kwa mwaka 2023 yamalizika kwa mafanikio makubwa huko Mbozi mkoani Songwe.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo (leo) Juni 30, 2023 kutoka wilayani Mbozi mkoani Songwe, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utafiti, Machapisho na Ubunifu wa OUT ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya NCAA, Dkt. Harrieth Mtae, amesema shughuli zote zilizoambatana katika maadhimisho ya siku kimondo duniani yamekwenda vizuri lakini mbio za zimondo zimefanya vyema.

“Nasema maadhimisho haya yamefana sana sababu katika mbio hizi za km 5, 10 na 21 yamepata washiriki wengi wa ngazi za kimataifa na kitaifa, kutokana na kufana kwa maadhimisho haya tunategemea taarifa za zao hili jipya la utalii wa anga zitazidi kusambaa sababu ni kitu ambacho hakijazoeleka hivyo jamii inapaswa kuhabarishwa juu ya utalii wa anga ili kuleta matoke chanya.” Amesema Dkt. Mtae

Pia, Kamishna Msaidizi Mwandamizi kutoka NCAA, Joshua Mwamkunda, akizungumzia katika kilele cha maadhimisho hayo, amesema kitendo tu cha wananchi wengi kufika kwa wakati mmoja katika maeneo ya kimondo hayo tayari ni mafanikio tosha kuhusu kueneza habari hizi za utalii wa anga na kimondo.

“Kitendo tu cha washiriki wa hizi mbio kutoka mikoa mbalimbali pamoja na wananchi wa maeneo jirani waliofika kujionea maadhimisho haya ni mafanikio tosha juu ya uhamsishaji na uelimishaji juu ya urithi wa anga na utalii wake, watu wengi wamefika hapa na wametembelea kimondo, wamepiga picha maana yake tayari wamefanya utalii wa ndani lakini kutuma picha mitandaoni hapo matangazo yanasambaa sehemu tofauti.” Amesema Kamishna Mwamkunda.

Aidha, alisisitiza kuwa lengo la maadhimisho haya ni kuelimisha, kuhamasisha na kuendeleza utalii wa anga na urithi wake hasa hivi vimondo vilivyopo nchini ili kuongeza watalii wa anga kutoka ndani na nje ya nchi na kuungana kwa vitendo juhudi za serikali katika kuhamasisha utalii nchini.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utalii, Ukarimu na Geographia wa OUT, Dkt. Halima Kilungu, amesema kuhamasisha wananchi kupenda utalii wa anga ni kuwafanya wapende mazingira hayo hivyo watashiriki katika kuyalinda mazingira ya anga dhidi ya uharibifu.

Maadhimisho ya siku ya anga duniani huadhimishwa Juni 30, kila mwaka ambapo kwa hapa nchini yamekuwa yakiadhimishwa katika mkoa wa Songwe ili kuhamasisha utalii nyanda za juu kusini kupitia kimondo kilichopo wilayani Mbozi mkoani Songwe. Taasisi mbili za NCAA na OUT wamekuwa wakishirikiana katika maadhimisho hayo nchini ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika kutangaza vimondo vilivyopo sambamba na zao jipya la utalii wa anga.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages