Breaking

Saturday, 8 July 2023

MASPIKA, WABUNGE WA SADC WAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA, WAFANYA ROYAL TOUR NGORONGORO, MCHENGERWA ASISITIZA MABORESHO MAKUBWA YAJA


Na John Mapepele

Maspika, Wabunge na Viongozi Wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika waliokuwa wakishiriki Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za SADC uliofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 3, 2023 jijini Arusha ambao umemalizika leo wametembelea Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio vya kipekee vya utalii vinavyopatikana nchini kufuatia wito alioutoa Mhe. Rais wakati wa ufunguzi.

Mara baada ya kuingia kwenye hifadhi hiyo viongozi hao wamefurahishwa na uzuri waliouona na kufafanua kwamba watakuwa balozi wema wa kutangaza uzuri wa hifadhi hiyo ili watu wengine kutoa maeneo mbalimbali duniani waje kujionea vivutio vya kipekee vilivyopo nchini.

Spika wa Bunge la Afrika Kusini Mhe. Nosiviwe Mapisa amesema Ngorongoro ni miongoni mwa hifadhi kubwa kwenye eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye kutangaza utalii wake ambapo amesema Afrika ya Kusini itajifunza kutoka Tanzania.

Naibu Spika wa Bunge la Botswana, Mhe. Pono Moatlhod amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi ya kipekee kabisa katika bara la Afrika ambayo imebarikiwa kuwa na vivutio vizuri vya utalii ambayo imekuwa ikipiga maendeleo kwa kasi.

“Tanzania ni nchi katika ukanda wa Afrika ambayo haina hatari zozote za kivita, mapigano, na ugaidi ni nchi yenye amani tele ambayo iinakua kimaendeleo kwa haraka.” Amesifia Mhe. Moatlhod

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua Tanzania kwenye sekta ya Utalii kupitia Royal Tour ambapo amefafanua kuwa kazi inayoendelea kwa sasa ni kuboresha na kuongeza miundombinu ili iweze kuhimili wimbi kubwa la wageni waoingia nchini.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuona kuwa sekta inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi ambapo amesisitiza kuwa kwa vivutio vingi na vizuri ambavyo vingine havipatikani katika nchi nyingi duniani Tanzania inatakiwa kuwa nchi inayoongoza Afrika na duniani kwa kuwa na wageni wengi na kufanya vizuri kwenye sekta.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha eneo ya utalii wa mikutano kwa kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya mikutano ya kimataifa ili wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali waweze kufanyia mikutano yao hapa nchini na wakimaliza waweze kutembelea maeneo yetu na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii.

Akiwahamasisha kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii wakati anafungua mkutano huo wa wabunge Mhe. Rais Samia aliwahakikishia wajumbe hao kuwa Arusha ni eneo la kitovu cha utalii wa kimataifa ambapo wanaweza kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika hifadhi na kufurahia vivutio hivyo ambavyo vingine havipatikani katika maeneo mengi duniani.

“Naomba niwahakikishie kwa wageni ambao ni mara ya kwanza kuja nchini, Arusha ni sehemu nzuri ya kitalii kwa ajili ya kujionea vivutio vya utalii vya kimataifa.” Amesisitiza Mhe. Rais

Aidha, alitoa wito kwa wajumbe hao kutembelea maeneo mengine ya Tanzania pindi wakimaliza mkutano huo kuwa ni pamoja na Zanzibar na maeneo ya kusini mwa Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages