Breaking

Thursday, 6 July 2023

KITUO CHA SAUTI YA JAMII KIPUNGUNI CHATUMIA UJASIRIAMALI KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

KITUO cha Sauti ya Jamii Kipunguni Ukonga Jijini Dar es Salaam, kimekuwa kikitumia Ujasiriamali katika harakati za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye jamii ambayo inawazunguka.

Akizungumza leo Julai 5,2023 wakati Kituo hicho kilipotembelewa na Wanajamii wa Vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka Mkoa wa Shinyanga na Dar es Salaam, ambao wapo katika Mafunzo ambayo yameandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP, Mwanakituo wa kituo hicho Bw.Juma Masanja amesema wamekuwa wakitumia Ujasiriamali kuwaleta jamii pamoja na kutoa elimu ya kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Amesema kituo hicho kimekuwa na utaratibu wa kukusanya taka na kuzibadilisha kuwa fursa hasa kutengeneza bidhaa ambayo kwa wakati huo inahitajika sokoni kama vile taka kuzibadili kuwa mkaa wa kupikia, taka zilizooza (Matunda) kutengeneza wadudu ambao ni chakula cha mifugo.

Aidha amesema wamekuwa na klabu za kupinga ukatili ndani ya jamii ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya ukatili katika maeneo ambayo yapo karibu na Kipunguni Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hayo amesema wamekuwa wakitumia kilimo cha mbogamboga kama sehemu ya kupinga ukatili wa kijinsia pale ambapo wanafanya kilimo na kukutana pamoja kwaajili ya kupeana taarifa .

Nae Mwanajamii wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kutoka Mkoa aa Shinyanga amesema kuwa maendeleo ambayo wameyaona Kipunguni, wamejifunza hivyo watakwenda kuhakikisha katika vituo vyao wanafanya maendeleo na kuhakikisha wanawaweka wanajamii karibu na kurahisisha kutoa elimu ya Kupinga Ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages