Breaking

Sunday 30 July 2023

DKT. MABULA AIPONGEZA ORYX GAS KUHAMASISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA, YATOA MITUNGI 500 BURE KWA MAMA LISHE ILEMELA

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula amesema hatua ya Kampuni ya Oryx Gas kutoa hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono kwani inaisadia Serikali kuhamsisha utunzaji mazingira nchini.

Katika kuendelea kutoa hamasa ya wananchi kutumia nishati safi ya kupikia, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imegawa bure mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa wanawake wajasiriamali ambao wanajishughulisha na shughuli za Mama Lishe Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi majiko hayo, Ilemela jijini Mwanza, Waziri Dk. Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela amesema mitungi na majiko hayo ya Oryx yametolewa kwaa Mama Lishe kwenye zote 19 za wilaya hiyo kulingana na shughuli zinazofanywa na Mamalishe wilayani humo.

“Tunaona namna ambavyo akinamama wanapata shida katika kutekeleza shughuli zao kwa haraka, katika mazingira mazuri, lakini tunahitaji kutunza mazingira yetu. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha huduma zote anazotoa kaanzia kwenye huduma za uchumi, kaja kwenye elimu lakini uwekezaji ameupa kipaumbele.

“Ukija katika huduma za jamii akina mama wengi wamekuwa wakihanagika kutafuta kuni na mkaa, wanakwenda kufyeka misitu.Tumetajiwa hadi kiwango cha uharibifu ambacho kimefanyika. Sasa tunapopata kampuni kama hizi ambazo ziko tayari kuwekeza katika afya na utunzaji bora wa mazingira yetu, lazima tuwashukuru,” alisema.

Alisema anaamini mitungi hiyo iliyotolewa ikiwa imejazwa gasi itakuwa chachu kwa wanawake hao kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia na pindi itakapokeisha gesi iliyomo wataendelea kuijaza.

“Gunia moja la mkaa linauzwa kati ya sh. 70,000 hadi sh. 70,000 na ukilitumia kwa kubana hauzidi wiki tatu au mwezi mmoja, sasa niambie ni mitungi ya gesi mingapi katika hilo gunia moja unalolipata? Ni mitungi mitatu ambayo itakulepeka hadi miezi mitatu," amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Araman Benoite, amesema kuwa wameendelea kuunga mkono juhudi za serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kutunza mazingira kwa kuhamasisha nishati safi ya kupikia.

“Katika mwendelezo huo wa kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama kwa kupikia, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited imekuwa mstari wa mbele kufikia azma hiyo, leo (jana) kampuni yetu imevitupia macho vikundi vya wafanyabiashara wa vyakula (Mama Lishe) Wilaya ya Ilemela kwa kuwakabidhi mitungi 500 ikiwa na gesi yake bure.

“Utoaji huu wa mitungi ya Oryx umefanikiwa kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Waziri Dk. Mabula. Malengo ya kampuni ni kuona mabadiliko katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa jamii ya Watanzania,” amesema.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Araman Benoite.

Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoite akizungumza wakati wa tukio la ugawaji mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Mama Lishe waliopo katika Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza

Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Peter Ndomba akitoa elimu ya matumizi salama ya mtungi wa gesi ya Oryx kabla ya mitungi hiyo kukabidhiwa kwa wanawake wajasiriamali wilayani Ilemela mkoani Mwanza



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages