Breaking

Tuesday, 4 July 2023

DKT. GWAJIMA KUIUNGANISHA SEKTA YA MADINI NA MAJUKWAA YA WANAWAKE



Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima amesisitiza kuwa ataiunganisha Sekta ya Madini na Majukwaa ya wanawake ili kupata uelewa kuhusiana na fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Julai 4, 2023 alipotembelea banda la Wizara ya Madini, Taasisi za wizara na wadau wake katika Maonesho yanayoendelea ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt.Gwajima amevutiwa na muundo wa utendaji kazi unaozingatia uwazi na usawa wa jinsia katika kutekeleza mipango ya maendeleo ndani ya Sekta ya Madini.

Kwa upande wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) amefurahishwa na ushirikishwaji na namna shirika hilo linavyowashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali za utafiti na uzalishaji madini na kuahidi kufika katika maeneo yao ya kazi ili kujionea utendaji kazi wao.

Amefurahia na kuipongeza STAMICO kwa kubuni na kuanzisha teknolojia ya nishati mbadala ya kupikia ambayo itasaidia kumtua mama kuni kichwani na kutunza mazingira.

Dkt. Gwajima ameipongeza Tume ya Madini kuhusu uwazi na usimamizi mzuri wa masoko ya madini. Aidha, akiwa katika banda hilo aliweza kupata fursa ya kufaham aina mbalimbali za madini na kupima baadhi thamani zake ili kujua uhalisia wa thamani hizo katika maabara ya Tume ya Madini iliyopo katika maonesho ya Sabasaba.












Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages