Na Nelson Shoo
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imechukua ubingwa wa michuano Maji Cup baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika katika uwanja wa Mao Tse Tung visiwani Zanzibar.
DAWASA imepata ushindi huo baada ya kumenyana na timu ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA).
Akizungumza baada ya timu ya mpira wa miguu DAWASA kuibuka na ushindi na kutwaa ubingwa huo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Kiula Kingu amewapongeza wachezaji wote pamoja na benchi la ufundi kwa jitihada zote walizofanya kuanzia maandalizi ya mashindano hadi kufikia kuchukua ubingwa huo.
"Nawapongeza wachezaji wote kwa kuipambania taasisi yetu katika mashindano haya hadi kufikia kuchukua ubingwa huu," ameeleza Kingu.
Kingu ameongeza kuwa ushirikiano mkubwa pamoja na juhudi za kila mchezaji ni chachu ya mafanikio haya ambapo DAWASA inachukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza.
Ushindi huu unaifanya DAWASA inayonolewa na Kocha Mkuu Mohammed Magali kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza tokea Michuano ya Maji Cup ilipoanzishwa mwaka 2021.
Kwa upande wake, kocha mkuu wa DAWASA, Ndugu Mohamed Magali alisema kuwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Kiula Kingu pamoja na Menejimenti nzima kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya kuelekea mashindano haya ya Maji Cup ndo chachu kubwa ya mafanikio haya.
"Tunaishukuru Menejimenti ya DAWASA inayoongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Ndugu Kiula Kingu kwa ushirikiano mkubwa aliyotupa kwanzia maandalizi ya timu, ushiriki wa timu katika mashindano na hatimaye kufanikiwa tumefanikiwa kuwa mabingwa." ameeleza Magali.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa fainali za kombe la Maji Cup 2023 ni Naibu Waziri Maji, Nishati na Madini Zanzibar Mhe. Naibu Waziri Shaaban Ali Othman.
Mashindano ya Maji Cup yaliasisiwa mnamo mwaka 2021 na mashindano ya sasa ni msimu wa tatu yanayoenda na kaulimbiu isemayo "Thamani ya Maji kwa Uhai na Maendeleo."