Breaking

Thursday, 20 July 2023

BODI YA WAKURUGENZI DAWASA YASHUHUDIA KASI MRADI WA BWAWA LA KIDUNDA

Bodi ya Wakurugenzi, Mamlaka ya maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Kidunda na kutoa wito kwa Mkandarasi kukamilisha mradi ndani ya muda uliopangwa ili kuleta manufaa kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA, Bw. Laston Msongole wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa  mradi huo unaotajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati nchini.

''Tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugharamia mradi huu mkubwa na muhimu kwa nchi yetu. Kama Bodi ya DAWASA ambao ni wasimamizi wakuu wa DAWASA kwa niaba ya Serikali, tumekuja kutembelea eneo la mradi kwa lengo la kujionea maendeleo kwani ni takribani siku 30 tangu uanze kutekelezwa rasmi na Mkandarasi.

Nikiri wazi kuwa kasi ya Mkandarasi ni ya kiridhisha na ametuonesha ni kwa kiasi gani amejipanda kutekeleza mradi ili kukamilika kwa wakati, ''
alisema Bw. Msongole.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, ndugu Kiula Kingu amesema ziara ya Bodi hiyo  katika mradi wa Kidundà ni kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi kwakuwa ndio wasimamizi wa Mamlaka kwa niaba ya Serikali.

"Ziara hii ya Bodi ya Wakurugenzi ni chachu ya kuona uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe Rais. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Shilingi Bilion 335 kuhakikisha mradi huu unakuwa mkombozi wa Wakazi wa Dar es salaam na Pwani hasa wakati wa kiangazi.”alisisitiza Bw. Kiula.

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda unatajwa kuwa muarobaini wa changamoto ya upungufu maji katika mto Ruvu ambao ndio chanzo kikuu cha maji kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani. Mradi unatarajiwa  kutekelezwa ndani ya Miezi 36, tangu Juni, 2023

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages