Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi wa maji Mbezi Kitopeni katika wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam utakaohudumia wananchi zaidi ya 30,000.
Akizungumza katika ziara ya kukagua mradi huo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA ndugu Kiula Kingu ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya Mbezi Makabe na Msakuzi Kusini ambao awali walikuwa wakipata kwa msukumo mdogo.
"Mamlaka imetekeleza Mradi huu ili kupunguza changamoto za huduma kwa wakazi wa Mbezi Kitopeni ambao umehusisha ujenzi wa kituo cha kusuma maji pamoja na tenki la lita elfu 90 na umegharimu kiasi cha shiling bilioni 1" alisema Ndugu Kingu.
"Tunategemea kuhudumia wakazi zaidi ya elfu 30,000 watanufaika na mradi huu na hadi mpaka sasa tayari wakazi elfu 4000 wameunganishiwa huduma." Alisema Ndugu Kingu.
Naye mmoja wa wanufaika wa mradi huo Bi. Zaina Said Juma mkazi wa Mbezi makabe ameishukuru DAWASA kwa kukamilisha mradi ambao umeondoa adha waliyokuwa wakipata kwa kutumia gharama kubwa kupata huduma ya maji ambayo usalama wake hauleweki.
"Nilikuwa na nunua maji ya boza hata mara tano kwa mwezi kwa gharama kubwa nilikuwa siamini kuna siku nitapata maji kutoka DAWASA"alisema Bi. Zaina
Kwa upande wa Meneja wa DAWASA mkoa wa kihuduma Ubungo, Mhandisi Edison Robert amesema kazi ya kuunganisha huduma kwa wananchi inaendelea katika maeneo ambayo mradi umepita na huduma ya maunganisho kwa mkopo kwa kipindi cha miezi 6 hadi 12 inatokewa pia
"Tunaendelea na kazi ya kulaza mabomba katika maeneo ya Mbezi Makabe na Msakuzi kusini ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi hivyo tunawasihi wajitokeze kuomba huduma" alisema Mhandisi Robert