NA WAF- BUNGENI, DODOMA
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitenga zaidi ya Bilioni 5.4 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika jengo la mama na mtoto META, katika hospitali ya Rufaa ya kanda nyanda za juu Kusini - Mbeya na tayari kupitia MSD vifaa hivyo vimepelekwa kwaajili ya usimikwaji.
Hayo yamesemwa leo Juni 12, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Suma Ikenda Fyandomo katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha kumi na mbili Mkutano wa 46, Jijini Dodoma.
Amesema, "katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya META ya Mkoa wa Mbeya."
Ameendelea kusema, jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya META limeanza kutumika na ufungaji wa vifaa tiba katika vitengo mbalimbali unaendelea na unatarajia kukamilika mapema Mwezi Julai 2023 ili wananchi wanaohitaji huduma za aina mbalimbali waendelee kunufaika na huduma hizo.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeendelea kuboresha huduma katika vituo vyote vya utoaji huduma ikiwemo hospitali ya kanda ya KCMC huku zaidi ya Shilingi 983,612,500 hutumika kila mwezi kwaajili ya kulipa stahiki na mishahara ya watumishi 905 waliopo katika hospitali hiyo.
Pia, Dkt. Mollel amesema, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya Dawa, vitendanishi na vifaa tiba ili kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma katika hospitali ya KCMC, huku kiasi cha Shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo na shilingi milioni 263.6 kwa ajili ya uendeshaji.
Sambamba na hilo, Amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa ufadhili wa masomo ya ubingwa bobezi kwa watumishi 15 wa kada za afya wa KCMC wanaosoma ndani na nje ya nchi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mollel amesema Wizara ya afya kwa kushirikiana na Wizara ya fedha na OR Utumishi zinaendelea na mchakato ili kuhakikisha hospitali za Rufaa za kanda-Mbeya, pamoja na KCMC zinakuwa taasisi jambo litalosaidia kuongezewa mgao wa uendeshaji na kuboresha huduma kwa wananchi katika vituo hivyo vya kutolea huduma.
Mwisho.