Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imesema haitafumbia macho vitendo vyovyote vya uhujumu wa miundombinu ya Maji na hatua kali ikiwemo faini na kifungo zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa DAWASA- Tegeta, Bi Victoria Masele wakati wa operesheni maalum katika kata ya Ununio na kubaini wizi mkubwa wa maji katika nyumba ya mkazi wa Mtaa wa Obama, (jina lake limehifadhiwa) ambaye amebainika kuhujumu miundombinu ya maji kinyume na sheria.
Victoria amesema kuwa imekuwa ni tabia ya baadhi ya Wananchi wachache kujiunganishia huduma ya maji kinyume na sheria na taratibu za Serikali zilizowekwa na hivyo sasa DAWASA imeanza ooeresheni maalum kuwabaini wote na kuwachukulia hatua.
"Nawasisitiza Wananchi kuwa kama unahisi kuna changamoto katika huduma, basi fika ofisi ya DAWASA iliyopo karibu nawe ili kuweza kuomba msaada wa kitaalamu." amesema Meneja Masele.
Ameongeza kuwa Mamlaka kwa nyakati mbalimbali imekuwa ikipata hasara kutokana na wananchi wanaohujumu miundombinu kwa kujiunganishia huduma ya maji kinyemela na kupeleka huduma hiyo kukosekana kwenye maeneo mengi ya jirani.
"Wananchi wengi katika eneo la Boko pamoja na Tegeta wamekuwa na tabia ya kujiunganishia huduma ya maji tofauti na utaratibu uliopo, hivyo imetulazimu kufanya operesheni ya kukagua miundombinu yetu kwa Wananchi tunaowahudumia." aliongezea Meneja Masele.
Katika msako huo, Mamlaka imembaini Mwananchi mmoja (jina limehifadhiwa) aliyekutwa amejiunganishiwa kinyemela huduma ya Maji nyumbani kwake na baada ya kubainika alikiri kosa na anatakiwa kulipa faini ya Tsh milioni 70.
Naye, Afisa Biashara DAWASA, *Wendeline Komba* amesema kuwa oparesheni hiyo itaendelea katika maeneo yote yanayohudumiwa na DAWASA na endapo watabainika basi hatua itakayochukuliwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Obama, *Ndugu Julius Nhundulu* ameipongeza DAWASA kwa jitihada za kuwabaini Wananchi wachache wanaofanya hujuma na kusisitiza kuwa serikali ya mtaa itasaidiana na Mamlaka kuwabaini na kuwafikisha katika katika vyombo vya sheria.
Sheria ya maji ya mwaka 2019 kupitia kifungu namba 5, inasema kuwa ni kosa kuchukua au kuchepusha maji kutoka kwenye miundombinu ya maji ambapo adhabu yake ni faini ya kiasi kisichopungua *Shiling 500,000/= hadi 50,000,000/=* au kifungo cha miezi 12 hadi miaka 5 au vyote kwa pamoja.