NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WADAU mbalimbali katika Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS) wameiomba Serikali kupitia wizara inapofanya mapendekezo ya bajeti wawe wanaangalia mapendekezo halisi kutoka kwa wananchi husika ambao watakaoguswa na bajeti.
Akizungumza katika semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazoandaliwa na TGNP Mtandao wakati wakitoa mapendekezo yao katika Bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2023-2024, Muwezeshaji Bi.Theresia Lianjala amesema yale mapendekezo ambayo serikali wamekuwa wakiyapendekeza wazingatie yale ambayo wananchi wamekuwa wakiyaibua kwasababu wao ndo huwa wanakuguswa.
Aidha Bi.Theresia ameshauri katika eneo la bajeti matumizi halisi yawe wazi "Mnataka kujenga matundu ya vyoo kadhaa, basi muonesha na mseme ni kiasi gani kitatumika katika ujenzi wa hayo matundu ya vyoo na wananchi kufahamu kiasi hicho kinatosha kwenye ujenzi huo ama hakitoshi". Amesema
Kwa upande wa washiriki wa semina hiyo, wamesema Serikali iende kuangalia miundombinu ya elimu ambayo haijakamilika ili waweze kuona ni kwa namna gani wanaweza kukamilisha na kuondoa kero ambazo zimekuwa zikitokea kwa sababu ya uchache wa miundombinu ya elimu.
Kenned Macha ambaye ni mshiriki wa Semina ameiomba serikali kuiangalia suala zima la miundombinu inayomuwezesha mlemavu wa viungo kupata huduma ikiwemo ujenzi wa vyoo mahususi kwaajili ya walemavu wa viungo.