Na Said Mwishehe
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)umetumia Maadhimisho ya Wiki ya Barcode(Nembo ya utambuzi) kitaifa kuendelea kuhamasisha Watanzania kujikita katika ufugaji nyuki kwa kuzingatia maelekezo yote muhimu sambamba na kuwa na vifungashio vyenye ubora unaokubalika.
Pia Wakala huo umetumia nafasi hiyo kuhamasisha wafanyabiashara wanaotaka kujihusisha na biashara ya asali na nta kufika kujisajili kwani huu ndio msimu wake ambao unaanza Julai mwaka huu hadi Juni 30 mwakani.
Akizungumza leo Juni 17,2023 kwenye Maadhimisho ya Barcode kitaifa yanayofanyika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam , Ofisa Ufugaji Nyuki, Masoko na Leseni wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Theresia Kamote amesema wameshiriki katika maadhimisho hayo kwasababu nao ni wadau wa Barcode.
“TFS tunayo asali yetu yenye Barcode inayoturuhusu kuingia katika aina yoyote ya masoko ambayo yako ndani ya nchi pamoja na nje.Pia tuko hapa kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii haswa wafugaji nyuki pamoja na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki.
“Hii ni fursa mojawapo ya kurasimisha biashara zao za mazao ya nyuki, tunaka asali yao iwe kwenye viwango vya ubora na tunaposema ubora sio ubora wa bidhaa peke yake bali ubora wa bidhaa upite viwango vya kibiashara,”amesema Kamote.
Ameingeza kwa hiyo wafanyabiashara wanapokuwa na Barcode wataweza kuingia katika masoko makubwa yakiwemo ya nje ya nchi , kwasababu Tanzania inazalisha asali kwenda katika nchi mbalimbali za Ulaya,Amerika, Asia na Afrika.
“Tuseme dunia nzima asali ya Tanzania inakwenda lakini inakwenda ikiwa katika mzigo mkubwa , haiendi katika bidhaa ya mwisho kwa ajili ya kumfikia mlaji moja kwa moja, hivyo tukiweza kurasimisha biashara zao inamaana wakiweka nembo ya utambuzi katika vifungashio vyao maana yake asali ikienda katika hayo masoko makubwa hata bei zitakuwa tofauti,”amesema.
Aidha amesema TFS wako kwenye maonesho hayo kwa ajili ya kuhamasisha wafugaji nyuki wafuge katika njia sahihi na bora.Nyuki wafuge katika maeneo ambayo hayajaathiriwa na kimikali zozote zile ili asali iwe ubora unaotakiwa hata katika masoko wanayopeleka.
“Kwa hiyo wanatakiwa kufuata kanuni zote za ubora wa mazao ya nyuki ili waingie katika masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi , lakini pia msimu huu ni usajili, TFS tunatoa elimu kuhusu usajili kuhusu mazao ya nyuki kwani hauwezi tu kuingia kufanya biashara ya mazao ya nyuki bila kufuata taratibu ambazo Serikali imeweka .
“TFS tunatumia sheria ya ufugaji nyuki pamoja na kanuni za ufugaji nyuki , kwa hiyo hizo sheria zinamtaka mfanyabiashara asajiliwe kwa hiyo tunatoa elimu hapa ya namna wanavyoweza kusajiliwa ili waingie katika biashara ya mazao ya nyuki.”
Kamote amesema msimu wa kufanya usajili unatarajia Julai 1,2023 kwa hiyo wanahamasisha kuhusu suala la utaratibu ambao Serikali imeuweka,”amesema.
Aidha amesema kila mwaka wanasafirisha asali tani 1500 na tani 700 za nta zinaenda katika nchi mbalimbali, kwa hiyo asali ya Tanzania bado inahitajika huku akizungumzia pia fursa za uwekezaji zilizopo katika ufugaji nyuki , utalii na misitu.
Kwa upande wake Ofisa Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Karim Solyambingu amesema taasisi hiyo iliyo chini ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutumia fursa ya maonesho na majukwaa mbalimbali kutoa elimu kwa umma inayohusu kile wanachokisimamia.
“Tumepewa dhamana ya usimamizi endelevu wa rasilimali misitu pamoja na rasilimali zitokanazo na ufugaji wa nyuki pamoja na utalii Ikolojia, TFS tuko nchi nzima na tunaendelea kutumia majukwaa haya kuzungumza au kukutana na wadau wetu na mwitikio umekuwa mkubwa.
“Tukiwa kwenye maonesho kama haya inakuwa rahisi wadau kutufikia kwa hiyo waliokuwa na matatizo ya upatikanaji wa vibali vya kusafirisha mkaa , vibali vya uvunaji wa mbao , vibali vya kuvuna magogo, wale ambao walikuwa wanahitaji kujua mbinu za sahihi za kuotesha miche ya miti , TFS ndio mahali pake , kwa hiyo tumekutana na wadau wetu wa kila siku, wale wanaotaka kuanzisha ufugaji wa nyuki ambao hawana mashamba sisi tunawaambia TFS tuna misitu ambayo ipo kwa manufaa ya watanzania wote,”amesema
Ofisa Ufugaji Nyuki, Masoko na Leseni kutoka Wakala wa Huduma za Misitu( TFS) Theresia Kamote (kushoto) akikabidhi moja ya jarida linalochapishwa na Wakala huo kwa moja ya wananchi waliofika kwenye banda la TFS wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Barcode kitaifa yanayofanyika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Ofisa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)Karim Solyambingu akizungumza sababu za wao kushiriki kwenye maadhimisho ya Barcode kitaifa yanayoendelea viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam
Theresia Kamote ambaye ni Ofisa Ufugaji Nyuki, Masoko na Leseni kutoka TFS akiangalia asali wakati wa maonesho hayo
Mmoja wa maofisa wa TFS akiendelea na majukumu yake wakati wa maonesho hayo