Breaking

Wednesday, 21 June 2023

TBS YAKAMATA BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU ZENYE THAMANI YA ZAIDI MILIONI 25 KANDA YA MAGHARIBI

BIDHAA za mafuta ya breki ya dot 3, nguo za ndani za mitumba na nyaya za umeme ambazo zimepigwa marufuku nchini zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 25 zimekamatwa kupitia operesheni maalum iliyoendeshwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi.

Operesheni hii maalum imefanyika katika Mikoa ya Rukwa na Kigoma, ambapo wakaguzi wa shirika hilo walibaini uwepo wa bidhaa hizo zilizopigwa marufuku kutumika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa operesheni hiyo, Afisa wa TBS, Elisha Meshack, alisema operesheni hiyo ya ukaguzi imeenda sambamba na utoaji elimu kwa wenye maduka yanayouza bidhaa hizo ili waweze kuzingatia matakwa ya viwango na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

“Operesheni hii ambayo imemalizika katika mikoa ya Rukwa na ni endelevu na lengo ni kuhakikisha soko la Tanzania linakua na bidhaa bora na salama kwa matumizi ya wananchi na mazingira” alisema Meshack.

Alitaja madhara ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kuvaa nguo vya ndani za mitumba zilizopigwa marufuku kuwa ni magonjwa ya ngozi pamoja na yale yanayoshambulia sehemu za siri.

Kwa madhara ya kutumia nyaya zilizopigwa marufuku, Meshack alisema ni kuunguliwa na vitu na hata kuweza kusababisha vifo.

Kuhusu madhara ya matumizi ya mafuta y breki aina ya dot 3, Meshack alisema yanawez kusababisha breki zikafeli na kusababisha ajali ambazo zinaweza kusababisha uharibifu wa mali na hata vifo.

Kwa upande wake Afisa Masoko wa TBS, Deborah Haule alisema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kukamata bidhaa zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni ishirini na tano katika operesheni hiyo na kusisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu.

“Operesheni hii ni endelevu na tutaendelea na ukaguzi wa bidhaa hafifu sokoni mpaka pale tukapojiridhisha kuwa Tanzania yetu ni salama na wafanyabiashara wanasimamia ubora wa bidhaa katika maeneo yote,” alisema Haule.

Haule alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kufuata matakwa ya viwango wanaponunua na kutengeneza bidhaa ili kujiepusha na hasara wanazoweza kupata pale bidhaa zao zitakapogundulika kuwa zina ubora hafifu na vile vile aliwasisitiza kuwasiliana na ofisi za TBS pale wanapoona wana mashaka na bidhaa yoyote.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wameomba elimu hiyo izidi kutolewa na kudhibiti wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza bidhaa ambazo zilipigwa marufuku.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mkoani Kigoma, Ibrahim Ramadhani, alipongeza kazi nzuri inayofanywa na TBS na kushauri utaratibu huo uendelee ili soko la Tanzania liwe na bidha zinazokidhi matakwa ya ubora.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages