Breaking

Friday, 23 June 2023

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA YASAIDIA MABATI, VYAKULA KAMBI YA WAZEE

Na Mwandishi Maalumu

OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH) imehitimisha maadhimisho wa Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kukabidhi msaada wa mabati, vyakula na vifaa mbalimbali vya nyumbani kwa makazi ya wazee, wenye ulemavu na wasiojiweza Nunge, Kigamboni, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ubinafsishaji Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Pili Mazowea waliwaongoza watumishi wa ofisi hiyo leo Ijumaa Juni 23,2023 kukabidhi misaada iliyopokewa na Ofisa Mfawidhi wa makazi hayo yenye wazee 21, Jacklina Kanyamwenge.

Akizungumza katika makazi hayo, Nyasama aliyemwakilisha Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema kama sehemu ya Serikali, uongozi wa ofisi umeona kuna umuhimu wa kurejesha kwa jamii kwa kusaidia wazee hao katika mahitaji yao ya kila siku, lakini pia kusaidia kuboresha mazingira wanayoishi yakiwemo majengo.

“Leo mko hivi, lakini tunajua kwa umri wenu mmesaidia mengi katika nchi hii. Nanyi ni sehemu ya jamii, mnastahili kuenziwa kwa kuhakikishiwa mahitaji muhimu,” alisema na kuongeza kuwa, kadri Mungu atakavyowezesha, ofisi na watumishi wake watazidi kuwakumbuka wazee hao.

Naye Jacklina alishukuru kutembelewa na watumishi na viongozi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuongeza kuwa kwao ni faraja kubwa, lakini pia msaada wao wa mabati ya kisasa utasaidia kukabiliana na hali ya uchakavu wa baadhi ya majengo.

Mmoja wa wazee hao, Sijali Mohammed akishukuru alisisitiza jamii isiwasahau kwani nao wanahitaji faraja.

Mbali ya kutembelea makazi ya wazee na kukabidhi misaada, viongozi na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina yenye jukumu la kusimamia uwekezaji mkubwa wa serikali wenye thamani ya Sh trilioni 70 kwenye taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa, kwa wiki moja waliungana katika kuhudumia wateja na wadau wa ofisi kwa kutenga eneo maalumu katika makao makuu ya ofisi, Mtaa wa Mirambo, Dar es Salaam.

Aidha, katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu inayosema; “Kufanikiwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika Kunahitaji Usimamizi wa Utumishi wa Umma Wenye Mtazamo wa Kikanda” watumishi walikumbushwa kushughulikia malalamiko ya wadau na wateja wanaofuata huduma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina na kutunza kumbukumbu ya namna wateja wa ndani na wa nje wanavyohudumiwa huku wakihakikisha kuwa wanatatua changamoto zao.
Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama akikabidhi msaada wa mabati ya kisasa kwa Jacklina Kanyam-wenge, Afisa Mfawidhi wa Makazi ya Wazee, Walemavu na Wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni jijini Dar es Salaam leo Juni 23, 2023. Mbali ya mabati, Nyasama pia alikabidhi vyakula, nguo, viatu, sabuni na kadhalika kwa niaba ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na watumishi wake waliotembelea makazi hayo ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wakifuatilia jambo walipotembelea na kukabidhi misaada mbalimbali kwa wazee wanaoishi katika makazi ya wazee, walemavu na wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni, Dar es Salaam, leo Juni 23, 2023 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki wa Utumishi wa Umma leo Juni 23, 2023.

(Na Mpigapicha Wetu).

Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama akifurahia jambo na Evelyne Mgaji, mmoja wa wazee wanaoishi katika makazi ya wazee, walemavu na wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni, Dar es Salaam baada ya uongozi wa ofisi hiyo na watumishi kukabidhi misaada mbalimbali ikiwamo mabati ya kisasa, vyakula vya aina mbalimbali, nguo, viatu, sabuni na kadhalika, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki wa Utumishi wa Umma leo Juni 23, 2023.
(Na Mpigapicha Wetu).

Watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wakiwa katika picha ya pamoja na wazee wanaoishi katika makazi ya wazee, walemavu na wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni, Dar es Salaam baada ya uongozi wa ofisi hiyo na wa-tumishi kukabidhi misaada mbalimbali ikiwamo mabati ya kisasa, vyakula vya aina mbalimbali, nguo, viatu, sabuni na kadhalika, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki wa Utumishi wa Umma leo Juni 23, 2023.

(Na Mpigapicha Wetu).

Watumishi katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sophia Makundi (kushoto) na Sawa Sinde wakimsaidia Evelyne Mgaji, mmoja wa wazee wanaolelewa kati-ka makazi ya wazee, walemavu na wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni jijini Dar es Salaam ili aweze kuungana na wenzake kupokea ugeni na misaada mbalimbali ikiwamo vyakula, nguo, viatu na sabuni vilivyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na watumishi wake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma leo Juni 23, 2023.

(Na Mpigapicha Wetu).

Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohammed Nyasama akikabidhi msaada wa chakula kwa Nuru Said Ally, mmoja wa wazee katika makazi ya wazee, walemavu na wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Msaada huo umetolewa na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo pia imetoa mabati ya kisasa wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, leo Juni 23, 2023.

(Na Mpigapicha Wetu)

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages