KATIKA kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi vifaa vya kutenganishia taka katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Juni 5,2023 mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria na Ufuatiliaji (NEMC), Bw. Hamadi Taimur ameipongeza hospitali hiyo kwa kuendelea kutunza mazingira na kuzitaka taasisi nyingine zikiwemo hospitali kuiga mfano huo.
“Ukiangalia hapa Muhimbili mazingira yake ni ya kijani hakuna taka zinazozagaa na hii imewezekana kutokana na hospitali kuwa na timu inayosimamia usafi wa mazingira ya hospitali, kwakweli hili ni jambo la kuigwa na tunawaasa wengine waje wajifunze hapa” amefafanua Bw. Taimur.
Bw. Taimur ameongeza kuwa NEMC inaamini kuwa vifaa vilivyotolewa leo vitasaidia kuendelea kuboresha shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira wa maeneo mbalimbali ya hospitali kwa kuwa hospitali inazalisha taka za aina mbalimbali ikiwemo taka hatarishi.
Akipokea msaada huo msaada huo Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Matengenezo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bi. Domiana John kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH ameishukuru NEMC kwa msaada huo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuendelea kuimarisha shughuli za usafi hospitalini hapa.
Bi. Domiana amesema kipaumbele cha hospitali ni usafi na usalama wa wadau mbalimbali wanaoingia na kutoka ndio maana imeendelea kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuepuka kuzagaa hovyo kwa taka kwa lengo la kuepuka magonjwa mbalimbali.