Breaking

Friday 9 June 2023

MRADI BWAWA LA KIDUNDA WATAMBULISHWA NGAZI YA KATA, VIJIJI

Na Fredy Mshiu


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeendelea na maandalizi ya utekelezaji mradi wa bwawa la Kidunda kwa utambulisho kwa Watendaji na viongozi wa Serikali za mitaa yote nufaika katika Halmashauri ya Morogoro.


Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha watendaji hao na DAWASA, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe Rebeca Nsemwa ameipongeza DAWASA kwa kufikisha elimu ya mradi kuanzia ngazi ya juu kwa maana ya mkoa hadi ngazi ya Kijiji.


"Niwapongeze sana DAWASA  elimu hii hawakuishia kwa Viongozi wa juu tu, sasa mpaka wawakilishi wa wananchi wanaenda kuufahamu mradi na kujua manufaa yake na hatua zote za utekelezaji". Alisisitiza



Mhe Nsemwa ameongeza kuwa mradi huu pindi utakapoanza wanufaika wa kwanza wa mradi ni wananchi waliopo ndani ya utekelezaji wa mradi na pembezoni ya mradi kwa kuwapatia fursa mbalimbali ikiwemo ajira mbalimbali hivyo kuinua uchumi wa wilaya ya Morogoro.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha aliyemwakilisha Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, CPA Sais Kyejo ameeleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo na watu wa eneo linalozunguka mradi na kuahidi DAWASA inatekeleza mradi na kukamilisha kwa wakati.


"Pamoja na haya yote, Mamlaka inaenda kutekeleza awamu nyingine ya zoezi la kulipa fidia kwa wahanga wa mradi huu ambapo kiasi cha Tsh Bilion 1.4 kitaenda kulipwa kama fidia." ameeleza CPA Kyejo.


Nae msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa bwawa la Kidunda Mhandisi Christian Christopher ameeleza taratibu muhimu za maandalizi ya utekelezaji wa mradi zipo hatua za mwisho kuanza June18,2023.


Ujenzi wa mradi wa bwawa la Kidunda utakaotekelezwa na fedha za Serikali kwa gharama za Shiling Bilioni 335.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages