Mkurugenzi mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji NIRC Bw. Raymond Mndolwa amewaasa wafanyakazi wa Tume kufanya kazi kwa ushirikiano na kuongeza bidii kwa kuzingatia weledi na uzalendo na kuweka mbele maslahi ya taifa ili kuchochea maendeleo ya nchi katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji.
Bw. Mndolwa ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano na wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya Tume jijini Dodoma amesema ushirikiano baina ya wafanyakazi ni matokeo chanya katika kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo.
"Tunatakiwa tuwe na mawasiliano, tuambizane turekebishane, tushirikishane, kanuni yangu mimi vitu vyote ntaweka juu ya meza nawaita wenzangu tunashauriana, tunakubaliana, twendeni na taratibu hizo za kushirikishana" alisema Mndolwa.
Aidha Mndolwa amewaasa watumishi hao kutumia vizuri rasilimali za serikali kwa maslahi ya taifa badala ya kutumia rasilimali hizo kwa matumizi binafsi ikiwemo magari ya Tume pamoja vifaa vingine vinavyotumika kurahisisha shughuli za taasisi.
Hata hivyo Mndolwa amesema katika kuboresha shughuli za ukusanyaji ada za huduma za umwagiliaji katika skimu zote nchini Tume imejipanga kununua magari katika kila skimu ili kurahisisha zoezi la utoaji elimu ya ada za huduma za umwagiliaji pamoja na ukusanyaji ada hizo kwa wakulima.
"Tunanunua magari ya skimu kila skimu itakuwa na gari na tutakuwa na maofisa wa skimu ili waweze kukusanya ada za huduma za umwagiliaji"
Aidha awali kabla ya mkutano huo Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa alifanya kikao na Wahandisi wa Mikoa kwa njia ya mtandao ambapo amewataka wahandisi hao pamoja na watumishi wa tume mikoa kuongeza kasi katika zoezi la ukusanyaji ada za huduma za umwagiliaji.
Imetolewa na
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji NIRC
05/06/2023
Dodoma.