***********
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA), Bw. Kiula Kingu amesema maandalizi ya mradi wa kihistoria wa ujenzi bwawa la Kidunda unaotegemewa kuanza Juni 18,2023 yapo katika hatua nzuri.
Bw. Kiula ameyasema hayo wakati wa ziara ya Menejiment ya DAWASA katika eneo la mradi huo unaojengwa katika kata ya Kidunda, Halmashauri ya Morogoro Vijijini. Mradi huu ni muhimu katika kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika mto Ruvu wakati wa Kiangazi.
“Mradi huu ni mradi wa kimkakati utakaowezesha mto Ruvu kuwa na maji ya kutosha mwaka mzima hivyo kuiwezesha DAWASA kutoa huduma stahiki za maji hata kunapotokea kiangazi cha muda mrefu", alisema na kuongeza kuwa, kupitia mradi huu fursa mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimazingira zitakuwepo ikiwemo na kusaidia kutunza ikolojia ya viumbe hai, kutoa ajira za muda mrefu na muda mfupi kwa zaidi ya watu 1000 na kufungua mwanya wa uchumi kwa wananchi wa maeneo ya Morogoro Vijijini kupitia shughuli mbalimbali za uvuvi na kilimo.
“Tumejiridhisha maandalizi muhimu ya usanifu yanaendelea hata kabla ya tarehe rasmi ya kuanza mradi huu, kwani mkataba huu unahusisha Usanifu na Ujanzi wa Mradi", Alisema.
Mkandarasi wa mradi ni kampuni ya Sinohydro Corporation Ltd ya China na mradi unatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miezi 36 (Miaka mitatu).
Hadi sasa kazi muhimu za maandalizi ikiwa ni pamoja na kupima sampuli za udongo, kujua uhimilivu wa miamba, nguvu za maji mtoni zimekamilika na kuonesha matokeo chanya. Aidha mkandarasi pia ameanza ujenzi wa kambi rasmi ya mradi, kambi ya vijana watakaoshiriki ujenzi na uandaaji wa vifaa na mitambo ya ujenzi.
Kwa upande wake, Msimamizi upande wa DAWASA katika wa mradi huu Mhandisi Christian Christopher Gava alisema utekezaji wa mradi huo wa kihistoria mbali na kuhifadhi maji lita billion 190, utasaidia pia kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 20.
“Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ni mahususi kwa ajili ya kusaidia kudhibiti Mto Ruvu wakati wa ukame kwa kuyahifadhi maji katika kipindi cha Masika ili yatumike kuhakikisha kuna mtiririko wa kawaida wakati wa kiangazi" alisema na kufafanua kuwa Bwawa likishajaa, litaweza kutiririsha lita zaidi ya lita billion 2 kwa siku na kuifanya DAWASA kuweza kuendelea kutoa huduma kupitia mitambo ya Ruvu juu na Ruvu Chini hata kipindi cha kiangazi yaani mwezi Septemba hadi Novemba.
Alibainisha kuwa taratibu zote za awali za kimkataba kabla ya kazi kuanza rasmi zimekamilika na kwamba mkandarasi ameelekezwa kuanza rasmi usanifu na ujenzi wa bwawa.
Vilevile alieleza kuwa ujenzi wa bwawa hilo lenye ujazo wa lita bilioni 190 unahusisha ujenzi wa tuta la urefu wa mita 870 litakalounganisha kilima cha Kidunda na kilima cha Makange, ujenzi wa jengo la kuzalisha umeme (power house) , ujenzi wa kituo cha kupokea na kuruhusu umeme yaani “switch yard “ , kujenga njia ya kusafirisha umeme kwa umbali wa Kilomita 101 ili kuingiza kwenye grid ya taifa katika kituo cha kupokea umeme Chalinze pamoja na ujenzi wa barabara kwa umbali wa kilomita 75 kuanzia Ngerengere mjini mpaka Kidunda.
Barabara hii imara ya kiwango cha changarawe itawezesha mitambo mizito kufikishwa katika eneo la bwawa lakini pia itasaidia kuunganisha maeneo mbalimbali jirani na bwawa na kuchochea ukuaji wa shughuli za usafiriahaji na maendeleo ya uchumi.
Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kidunda unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya kiasi cha Shilingi Bilioni 335 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Juni 2023 hadi Julai 2026.