Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza mazao rasmi matatu ya utalii ambayo hayapatikani nchi yoyote duniani isipokuwa Tanzania na kuwaomba watanzania kuyatumia na kuyatangaza ili wageni kutoka sehemu mbalimbali kuja kuona.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa na Katibu Mkuu, Dkt Hassan Abbasi pamoja na Menejimenti ya Bodi ya Utalii nchini kumtangaza Mwanamitandao ya kijamii maarufu nchini na duniani Nicholas Reynolds maarufu kama Bongozozo ambaye ana mtandao mpana unaojumuisha mabloger mbalimbali wa kimataifa wanaofikia watu zaidi ya milioni 100 duniani.
Waziri Mchengerwa ameyataja mazao hayo matatu ya utalii ambayo hayapatikati sehemu yoyote duniani isipokuwa Tanzania kuwa ni pamoja na tukio la msafara wa Wanyama Numbu katika Hifadhi ya Serengeti maarufu kama Great Migration, tukio la kutembea kwa miguu kwa wageni katikati ya Hifadhi ya Ruaha umbali wa takribani kilomita hamsini na kuwepo kwa msafara wa makundi makubwa na kuweka makazi kwa samaki mkubwa kuliko wote duniani Potwe maarufu kwa jina la Papa Usingizi katika Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia.
Amefafanua kuwa mazao yote haya matatu hayapatikani mahali popote duniani isipokuwa Tanzania ambapo amesema pamoja na kuwepo lakini bado watu wengi hawayatambui kwa kuwa hayajatangazwa kikamilifu hiyo kutoa wito kwa Bodi ya Utalii nchini kutoka na kutangaza mazao haya kikamilifu.
“Ndugu zangu ni vizuri kutambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani na ya kwanza Afrika kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini havijatangazwa hivyo nitoe wito kwa watanzania wote kuwa wazalendo na mabalozi wa kutangaza na kuthamini urithi huu tuliopewa na Mwenyezi Mungu” amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Aidha, amemwomba Bongozozo kuwa balozi mzalendo na bora wa Tanzania ili kutumia umaarufu na mtandao wake kuutangaza utalii wa Tanzania kila kona ya dunia ambapo ameitaka Bodi ya Utalii nchini kupitia orodha ya mabalozi wa heshima kuona wale wasiofanya kazi na kuwaondoa ili kubaki na wachapakazi.
Kwa upande wake Bongozozo, raia wa Uingereza ambaye ameoa na kuishi Tanzania kwa muda mrefu ameahidi mbele ya Waziri wa Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, kuwa atatumia ipasavyo ushawishi wake duniani kuutangaza utalii wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii nchini, Dkt. Glladstone Mlay amesema kwa sasa Bongozozo anaanza ziara yake kutangaza vivutio vya utalii kusini mwa Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa utangazaji utalii kusini mwa Tanzania (Tanzania’s Southern Circuit Marketing and Promotion Strategy 2021-2026) ambao uliandaliwa kupitia mradi wa REGROW na kuzinduliwa Septemba 2022 Mkoani Njombe umetaja njia mbalimbali za utangazaji utalii wa Kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kutumia; watu maarufu/mabalozi wa hiyari, utangazaji kwa njia ya mtandao (Digital and Social Media Marketing) vyombo vya habari, safari za mafunzo na kushiriki katika maonesho ya kibiashara (Travel Trade Marketing) ,matukio.
“Leo tumekutana hapa ili kuwajulisheni kuwa kuna ziara ya kimafunzo (Fam Trip ) ya BW. NICHOLAS REYNOLDS maarufu kama Bongozozo, raia wa Uingereza (Enland) kuanzia tarehe 13 Juni ,2023 hadi tarehe 24 Juni ,2023 katika mikoa ya nyanda za juu kusini, Tanzania.” amefafanua
Ameongeza kuwa Bw. Nick Reymonds (Bongozozo), ni Balozi wa hiari wa utalii (Good will Tourism Ambassador) tangu mwaka 2019 ambapo amekuwa mstari wa mbele katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ikiwa ni pamoja na kutumia michezo ndani na nje ya nchi, kutumia bloggers wenzake maarufu kama (Drew Binsky) na mbinu nyingine mbalimbali katika kuitangaza Tanzania kikanda na Kimataifa.
Amesema ziara hiyo itampa fursa yeye kama balozi kufahamu vizuri vivutio kwa uhalisia wake ili kumrahisishia katika utangazaji wake katika maeneo mbalimbali ambayo atatembelea katika utangazaji wake.
Aidha amesema katika kipindi hiki cha takribani wiki mbili za FAM TRIP ya Bongozozo, mawakala wa utalii wameandaa vifurushi (Package) za kutembelea vivutio hivyo atakavyotembelea Balozi huyu katika Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Pori la Akiba la Mpanga Kipengere Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Waziri Mchengerwa amewanakaribishwa watanzania wote kujumuika na Bongozozo katika kutembelea vivutio vya utalii vya nyanda za juu kusini ambavyo kwa sasa Serikali imeongeza nguvu kupitia mradi wa Usimamizi Rasilimali za Maliasili kwa Utalii na endelevu (REGROW) na kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kutangaza Tanzania kupitia Filamu pendwa ya “Tanzania The Royal Tour”.