Breaking

Tuesday, 13 June 2023

MAOFISA TPA, WAZIRI MAMBO YA NDANI JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO WAJADILIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO BIASHARA

Na Mwandishi Wetu

UJUMBE wa Tanzania ukiongozwa na Kaimu Konseli Mkuu Asha Mlekwa, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Usafiri Majini kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mussa Shashura pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Jimbo la Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Dieudonne Kasaka.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Juni 13, 2023 kwenye ofisi za Kasaka zilizopo Mjini Kalemie ambapo ujumbe wa Tanzania na mwenyeji wao pamoja na mambo mengine wamejadiliana kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa nchini Tanzania.

Baadhi ya miradi hiyo ni uboreshaji wa Bandari ya Kigoma, ujenzi wa Reli ya SGR, ujenzi wa Meli katika Ziwa Tanganyika na kuanza kutumika kwa Bandari ya Karema iliyopo Mkoani Katavi.

Aidha, ujumbe huo unatarajia kutembelea eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu ya Kasambondo lenye ukubwa hekta 25 lililopo Mjini Kalemie, Bandari itakayorahisisha na kuwezesha mnyororo wa biashara kwa shehena ya mizigo.

Kwa mujibu wa maelezo ni kwamba mizigo hiyo ni ile inayoingia na kutoka DRC kupitia Bandari ya Kalemie iliyopo Jimbo la Tanganyika kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Kigoma, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Makubaliano Maalum (MoU) ya ushirikiano kati ya Nchi hizi mbili yaliyofanyika tarehe 19 Julai, 2022.

Aidha imeelezwa kwamba kurahisisha usafirishaji wa shehena za mizigo kuingia na kutoka DRC kupitia Bandari ya Kalemie kutoka Bandari ya Dar es Salaam na Kigoma, TPA inaendelea na mpango wa kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu utakaohusisha Bandari ya Kalemie, Moba na Bandari kavu ya Kasambondo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages