Breaking

Thursday, 15 June 2023

MABORESHO MAKUBWA KWENYE UTALII HAYA HAPA


Na John Mapepele


Serikali inakwenda kufanya marekebisho ya ada na tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuvutia uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba katika hotuba yake wakati akiwasilisha bungeni leo mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24 katika eneo la Maboresho ya mfumo wa kodi, ada, tozo na hatua nyingine za mapato.


Mhe. Nchemba ameyataja maeneo ambayo Serikali imezingatia kuwa ni pamoja na kufuta ada ya kupanga na kurudia kupanga (grading and regrading) huduma za malazi zilizo nje na ndani ya maeneo ya hifadhi.

Kupunguza viwango vya Ada ya leseni ya biashara ya utalii katika huduma za malazi zinazomilikiwa na Watanzania kutoka dola za kimarekani 2,500 hadi dola za kimarekani 1,500 kwa hoteli za nyota tano; dola za kimarekani 2,000 hadi dola za kimarekani 1,000 kwa hoteli za nyota nne; dola za kimarekani 1,500 hadi dola za kimarekani 500 kwa hotel za nyota tatu; dola za kimarekani 1,300 hadi dola za kimarekani 300 kwa hoteli za nyota mbili; na kutoka dola za kimarekani 1,000 hadi dola za kimarekani 200 kwa hoteli za nyota moja.
Pia kupunguza Ada ya Leseni ya Utalii kwa huduma za malazi ambazo hazijakaguliwa na kupangwa katika viwango vya ubora (ungraded accommodation) nje ya maeneo ya hifadhi kutoka dola za kimarekani 1000 hadi dola za kimarekani 300; huduma ya malazi zinazopatikana katika makazi ya mtoa huduma (homestay) kutoka dola za Kimarekani 400 hadi dola za kimarekani 100; na hosteli kutoka dola za kimarekani 400 hadi dola za kimarekani 200.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages