Breaking

Sunday, 18 June 2023

ELIMU YA VIPIMO KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA BARCODE KITAIFA

Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kushiriki kwenye maadimisho ya Siku ya Barcode Kitaifa inayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja kuanzia tarehe 15 – 19 Juni, 2023.

Dkt. Dorothy ameeleza kuwa wajasiriamali wanahitaji kuendelea kupatiwa elimu kuhusu vipimo ili waweze kuongeza thamani ya bidhaa zao kwa kuandika kwa usahihi alama za vipimo kwenye bidhaa na pia kuweza kufungasha bidhaa zao kwa kutumia vipimo vilivyo sahihi na vilivyo hakikiwa na Wakala wa Vipimo ili wasipunjike na wasiwapunje wateja wao kwa lengo la kufanya biashara kwa usawa na haki.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo Bi. Rehema Michael ambaye ni Afisa wa Wakala wa Vipimo amesema ufungashwaji wa bidhaa za Wajasiriamali unazidi kuimarika mara kwa mara na hii inaonesha kuwa wajasiriamali wetu wanaelewa elimu tunayowapatia na kama Wakala wa Vipimo tutaendelea kutoa elimu hiyo na ushauri wa kitaalamu mara kwa mara ili kuhakikisha bidhaa zinakuwa na vipimo sahihi na zinafungashwa kwa kutumia vipimo sahihi vilivyo hakikiwa.

Kwa upande wake mfanya biashara wa dagaa za Fahari ya Mwanza Bi.Jesca Kweba amesema elimu aliyoipata kwenye banda la Wakala wa Vipimo itamsaidia sana katika ufungashaji wa dagaa zake na kuhakikisha hajipunji wala kuwapunja wateja wake kwani hapo awali alikuwa hajapata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo.

Wakala wa vipimo inawakaribisha Wananchi wote endapo watakumbana na changamoto za vipimo kwenye maeneo mbalimbali kutembelea Ofisi ya karibu ya Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kupata msaada au kupiga namba ya bure ya 0800 110097 kwa msaada zaidi.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages