Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea na operesheni ya kukamata, kuharibu na kuteketeza dawa za kulevya aina ya bangi katika wilaya ya ARUMERU mkoani Arusha na kufanikiwa kukamata jumla ya gunia 731 za bangi kavu pamoja na kuteketeza hekari 308 za mashamba ya bangi.
Operesheni iliyofanyika jana tarehe 01 June, 2023, katika kijiji cha Lesinoni, jumla ya gunia 249 za bangi kavu zilikamatwa huku hekari 207 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku operesheni iliyofanyika tarehe 31 Mei 2023, katika kijiji cha Kisimiri juu, Mamlaka ilikamata gunia 482 za bangi na kuteketeza jumla ya hekari 101 za mashamba ya bangi. Watuhumiwa 9 wamekamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa Umma iliyotelewa na Kamishna Jenerali Aretas Lyimo Leo tarehe 02 June, 2023;
operesheni hii imefanyika kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini. Operesheni hizi zimefanyika siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambayo iliitaja mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Manyara kujihusisha na kilimo cha bangi kwa kiasi kikubwa.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha kilimo cha bangi na mirungi kinatokomezwa kabisa na wananchi kujikita katika kilimo cha mazao mbadala ya biashara na chakula.