NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) limeanza na zoezi la kawaida la usajili wa watoa huduma binafsi na utoaji vibali vya uendeshaji wa magari yanayotoa huduma za usafi wa Mazingira (faecal sludge Emptier) ambapo zoezi hilo linafanyika eneo la mabwawa ya Vingunguti bila gharama yoyote.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo leo Juni 8,2023 Afisa Biashara Magari DAWASA Bi.Mwajuma Hamza amesema zoezi hilo ni endelevu na linafanyika mwezi Juni kila mwaka kwa kushirikiana na watu binafsi.
Madhumuni ya zoezi hilo ni kupata data zao ili kuweza kuwafahamu ni watu gani ambao wanafanya nao kazi ili waweze kutoa huduma pamoja nao katika kuhakikisha usafi wa mazingira unafanyika kikamilifu kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.
"Leo tumeanza usajili na utaendelea ambapo ndani ya wiki moja tutakuwa hapa ndani ya wiki moja katika eneo hili la mabwawa Vingunguti lakini tutaendelea katika ofisi zetu Kisutu kwa muda wa mwezi mmoja". Amesema
Amesema watakuwa wanasajili magari ambayo yapo lakini pia wanakaribisha magari mapya kusajili na kuweza kutambuliwa na DAWASA katikauendeshaji wa shughuli zao za utoaji huduma za usafi wa mazingira.
"Kwa magari yaliyosajiliwa awali, tunawaomba kufika kwaajili ya kufanyiwa uhakiki na ujazo wa gari pamoja na fomu halisi ya ujazo kutoka kwa Wakala wa Vipimo (WMA) na nakala yake". Amesema Bi.Mwajuma.
Pamoja na hayo amesema baada ya muda wa usajili kuisha, yeyote atakayekutwa anatoa huduma ya unyonyaji na usafirishaji wa majitaka katika eneo la huduma DAWASA bila kibali hai cha uendeshaji atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hata hivyo amesema magari yote yatakayopata vibali vya uendeshaji wa huduma yatabandikwa stika za DAWASA.
Mrisho Mataula ambaye ni mwendeshaji wa magari yanayotoa huduma unyonyaji na usafirishaji wa majitaka amewapongeza DAWASA kwa zoezi la usajili ambalo wanaliendesha kwani itawasaidia kwa kiasi kikubwa kutambulika na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
Amesema wamekuwa wakishirikiana na DAWASA kwenye maeneo ya shughuli zao hivyo kwa zoezi hilo la usajili litaweza kusaidia kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara na kuondoa baadhi ya kero ambazo zimekuwa zikitokea kwao.
Nae Alex Masumbuko ambaye pia ni mjumbe wa majitaka amewaomba DAWASA kuendesha shughuli hiyo pasipokuwa na usumbufu kwao kwani wanapoendesha zoezi hilo na wao wanakuwa wanaendelea na shughuli yao ambayo wanaifanya katika kutoa huduma.