ZAIDI ya watu 260 wanaripotiwa kufariki dunia nchini India na wengine 900 wamejeruhiwa baada ya treni mbili za abiria na nyingine ya mizigo kugongana huko katika Jimbo la Odisha lililopo Mashariki mwa nchi hiyo.
Ajali hiyo imetokea siku ya Ijumaa Juni 2, 2023 katika Wilaya ya Balasore katika Jimbo la Odisha inatajwa kuwa tukio baya zaidi la reli nchini India katika takribani miaka 20 iliyopita.
Mtendaji Mkuu wa Jimbo la Odisha, Pradeep Jena amesema, idadi ya waliokufa kufuatia ajali hiyo ya Ijumaa inatarajiwa kuongozeka.
Aliongeza kuwa, zaidi ya magari 200 ya kubebea wagonjwa yalikwenda katika eneo la ajali katika wilaya hiyo na madaktari wa ziada 100, ikiwa ni kuwaongezea nguvu wengine 80 ambao tayari walikuwepo katika eneo la tukio.
Madaktari hao walikuwa wanawajibika kuwapeleka majeruhi hospitalini na kuwahudumia wale ambao bado walikuwa kwenye eneo la tukio.
Wanajeshi wa jeshi na helikopta za jeshi la anga walijiunga katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada huo pamoja na viongozi wa eneo hilo.
Picha za video zilionesha waokoaji wakipanda juu ya treni iliyosongamana kutafuta manusura, huku abiria wakiomba msaada na kulia karibu na mabaki hayo.
Ajali hiyo iliyohusisha mgongano kati ya treni hizo ulitokea takribani saa 7 mchana kwa saa za ndani (13:30 GMT) siku ya Ijumaa wakati treni ya Howrah Superfast Express inalotoka Bengaluru hadi Howrah, West Bengal, lilipogongana na Coromandel Express inayotoka Kolkata hadi Chennai.
Debabrata Mohanty, mhariri katika gazeti la Hindustan Times, ameiambia Al Jazeera kwamba mabehewa manne ya kwenye treni iliyoondoka kutoka Kolkata yalitoka kwenye njia muda mfupi kabla. "Hakuna anayejua jinsi ilivyokuwa, lakini ilikuwa ikisafiri karibu kilomita 100 kwa saa," alisema.
Muda mfupi baadaye, treni iliyokuwa ikitoka Bengaluru iligonga mabehewa mawili ya reli yaliyoacha njia. "Lakini majeruhi wengi walitokea kwa sababu treni hii iliacha njia, si kwa sababu ya treni mbili kugongana," Mohanty aliongeza.
Operesheni ya kina ya utafutaji na uokoaji imeanzishwa, ikihusisha mamia ya wafanyakazi wa idara ya zima moto, maafisa wa polisi na mbwa wa kunusa. Timu za Kikosi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Maafa pia zilikuwepo eneo hilo.
Mtu mmoja aliyenusurika alisimulia namna alivyonusurika na jinamizi hilo la ajali alipokuwa ameamka wakati gari moshi alilokuwa amelala lilipopinduka.
"Usingizi wangu ulikatika na watu 10-15 waliniangukia," aliwaambia waandishi wa habari, alipokuwa ameketi chini gizani, hatua mbali na eneo la ajali.
"Niliumiza mkono na shingo yangu...niliona mtu amepoteza mkono wake, mtu amepoteza mguu...nilitoka pale na tangu wakati huo nimekuwa nikikaa hapa."
Juni 2, 2023, mamia ya vijana walijipanga nje ya hospitali ya serikali huko Odisha Soro ili kutoa damu. "Binafsi nina deni na ninashukuru kwa kujitolea na wote ambao wametoa damu kwa sababu nzuri," Jena aliandika kwenye tweet.
Jena aliielezea kama, "hii ni ajali mbaya na ya kutisha iliyohusisha treni tatu, treni mbili za abiria na treni moja ya mizigo".
Chanzo cha ajali hiyo kilikuwa kinachunguzwa, alisema Amitabh Sharma, msemaji wa Shirika la Reli la India. Taarifa za ajali hiyo hazikufahamika mara moja, wala mlolongo wa matukio hayo.
Waziri Mkuu wa Odisha, Naveen Patnaik ambaye anatarajiwa kuzuru eneo hilo leo alisema kipaumbele ni "kuondoa waliojeruhiwa na kuwapatia huduma hospitali. Hilo ndilo jambo letu la kwanza, kutunza walio hai."
Ripoti zinaonesha kuwa, mamia ya ajali hutokea kila mwaka kwenye reli ya India, huku nyingi zikilaumiwa kwa makosa ya kibinadamu au vifaa vya kuashiria vilivyopitwa na wakati.
Zaidi ya watu milioni 12 hupanda treni 14,000 kote India kila siku, wakisafiri kwa kilomita 64,000 (maili 40,000) ya njia.
Sudhanshu Mani, meneja mkuu wa zamani wa Shirika la Reli la India, aliiambia Al Jazeera kwamba uwekezaji umeingia katika matengenezo ya njia na hatua zingine za usalama katika miaka ya hivi karibuni.
"Ajali ya leo ni ya kusikitisha sana," Mani alisema, akiongeza kuwa majeruhi watakuwa wengi kutokana na idadi ya watu kwenye treni.
"Lakini idadi ya ajali imepungua na kuna miradi iliyopo njiani ya kuboresha usalama zaidi," alisema. Hakukuwa na uthibitisho rasmi wa jumla ya idadi ya abiria kwenye treni.
Maafa mabaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na moja la Oktoba 2018, wakati treni ilipita juu ya umati wa watu waliokuwa wakitazama fataki wakati wa tamasha la kidini nje kidogo ya Amritsar jijini Punjab hali iliyosababisha vifo vya takribani watu 60 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Takribani watu 146 waliuawa Novemba 2016, wakati treni ya abiria iliyokuwa ikisafiri kati ya miji ya Indore na Patna ilipoteleza kutoka kwenye reli. Zaidi ya watu 200 walijeruhiwa katika ajali hiyo.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alisema Ijumaa kuwa, shughuli za uokoaji zinaendelea na "msaada wote unaowezekana" ulikuwa ukitolewa kwa wale walioathiriwa.
Modi aliongoza mkutano wa ngazi ya juu leo na alitarajiwa kuzuru eneo la ajali baadaye mchana, pamoja na hospitali ya Cuttack ambako wengi wa majeruhi walikuwa wakitibiwa, shirika la habari la ANI liliripoti.
Waziri wa Reli Ashwini Vaishnaw, ambaye alikuwa akikimbilia eneo la ajali siku ya Ijumaa, alitweet: "Nitachukua hatua zote zinazohitajika kwa operesheni za uokoaji."
Vaishnaw pia alitangaza fidia ya takribani rupia milioni moja (dola 12,000) kwa familia za waliofariki, dola 2,400 kwa wale waliopata majeraha mabaya na dola 600 kwa watu walio na majeraha madogo. (Al Jazeera/Mashirikia/ DIRAMAKINI).