Breaking

Saturday, 6 May 2023

SIMBACHAWENE-TUMIENI MAFUNZO MLIYOYAPATA KAMA CHACHU KATIKA UTENDAJI WENU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amewataka wahitimu wa mahafali ya sita ya taasisi ya Uongozi kutumia mafunzo waliyopata kama chachu katika utendaji wao wa kazi na kuhakikisha wanaongoza jamii kwa maadili yaliyomema.

Pia amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kujiepusha na vitendo vya rushwa,matumizi mabaya ya uongozi na ubadhirifu wa fedha katika utendaji wao wa kazi.

Akizungumza kwenye Mahafali hayo,yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Waziri Simbachawene aliyekuwa Mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali nchini yanalenga kuboresha utendaji.

"Mtakubaliana nami kuandaa na kuendeleza viongozi sio jambo rahisi, kuna kila haja ya kuandaa viongozi kwa mafunzo mbalimbali ili kuwa na viongozi bora.Mwalimu Nyerere alisema nchi inahitaji Watu, Ardhi, siasa safi na Uongozi bora , hivyo ni muhimu kuandaa viongozi kwa kupatiwa mafunzo ya uongozi.

"Jambo ambalo linatuhimiza kuandaa viongozi bora ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, sensa inaonesha kuna watu milioni 61, kwa wingi huu tunahitaji kuandaa viongozi ambao watasimamia rasimali watu, hivyo ni jukumu letu kama taifa kuhakikisha tunajenga uongozi bora katika kusimamia rasilimali watu na kuleta maendeleo endelevu,"amesema Waziri Simbachawene.

Aidha amewapongeza wahitimu wote na kwamba sasa wanakwenda kukuza na kuimairisha utawala bora unaotenda haki na kuwataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha wanamsaidia Rais Samia Suluhu Hassan ambaye uongozi wake umeendelea kuiletea heshima nchini.

"Tumekuwa na nchi yenye utulivu ambayo inavutia wengi, hivyo ni muhimu kuwa na viongozi ambao watasimamia nchi yetu.Pia nimefarijika uwepo wa programu ya viongozi wanawake ambayo ni muhimu katika kujenga usawa wa kijinsia na kuwa na maendeleo endelevu.

"Hata hivyo bado kuna changamoto ya ufinyu wa wanawake katika nafasi za uongozi, hivyo ni lazima kuendelea kujengewa uwezo na Viongozi wanawake mnaohitimu nendeni makasaidiane na viongozi wanaume ili maarifa mliyoyapata yakalete suluhu na kuleta maendeleo ya nchi yetu,"amesema.

Pia amesema ili kufikia malengo ya uchumi ushirikiano wa sekta za umma na binafsi ni muhimu sana, hivyo ametoa mwito kwa Taasisi ya Uongozi kuangalia namna ya kujenga ushawishi kwa viongozi wa sekta binafsi kushiriki kwenye mafunzo hayo na bahati nzuri wameanza na ndio maana leo kuna viongozi wa taasisi binafsi wamehitimu

Pamoja na hayo ameishauri Taasisi ya Uongozi iendelee kuwatumia viongozi wastaafu ambao wana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi na wakipata nafasi hiyo watakuwa wanapata nafasi ya kuendelea kutoa maarifa yao na kurithisha kwa wengine.

"Ni vema wakawa wanapa nafasi ya kufundisha hata kila baada ya miezi mitatu, wakija hapa wanafurahi, hivyo tuwatumie , maana wamestaafu lakini wamebobea kwenye uongozi, hivyo uwekwe utaratibu mzuri wastaafu wawe wanafundisha."

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ikulu Mululi Mahendeka amesema ni muhimu kwa serikali kuendelea kuwajengea uwezo viongozi wake na kwamba imekuwa ikiongeza bajeti kwa taasisi hiyo kila mwaka ili iwe na uwezo wa kuendelea kutoa mafunzo hayo.

Awali Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu 2023 jumla ya viongozi 15000 wamapata mafunzo ya kozi mbalimbali kwenye taasisi hiyo na matarajio yao ni kuona viongozi wengi zaidi wanajiunga na kupata mafunzo.

Pia amesema programu 200 tofauti zimetolewa kwa viongozi wa kada mbalimbali ambao wamepita kwenye taasisi hiyo lakini viongozi 8000 wameshiriki shughuli za taasisi kwa nyakati tofauti.

Pamoja na hayo amesema wameona kuna haja ya kuwa na programu maalum ya kozi kwa Viongozi wanawake huku akifafanua programu hiyo inakwenda kuwajengea uwezo viongozi hao na hatimaye kutoa fursa ya kushiriki kwenye nafasi za uongozi.

"Takwimu zinaonesha duniani ni asilimia 22 ya viongozi wanawake walioko kwenye nafasi za maamuzi na ili kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi itafikiwa ifikapo mwaka 2050, hivyo uwepo wa programu hii ya viongozi wanawake ni muhimu."amesema Singo.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Zainab Said ameipongeza Taasisi ya Uongozi kwa kuandaa programu ya viongozi wanawake kwani inakwenda kupanua wigo wa kukua na kusonga mbele katika uongozi wao ikiwemo katika nafasi za maamuzi.

Amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kusaidia viongozi kujifunza masuala ya uongozi wakiwemo Viongozi wanawake kwa kuwapa nafasi ya kujifunza masuala ya uongozi.

''Natumia nafasi hiyo kuipongeza taasisi hiyo kwa kuona haja ya kuwa na programu kwa wanawake ambayo inaleta mwanga mzuri wa kuwaongoza katika utumishi wao,''amesema na kuongeza.

"Nimefurahishwa na Taasisi za Uongozi kuandaa mafunzo kwa ajili ya viongozi wanawake na mafunzo hayo yanaongeza wigo wa wanawake kuteuliwa,ni vizuri akina mama wakaendelea kujumuishwa kwenye ngazi ya maamuzi,itakuwa vizuri zaidi kama kutakuwa na usawa katika kutoa maamuzi,''amesema

Aidha amesema takwimu bado zinaonesha kuwa kuna idadi ndogo ya wanawake katika nafasi za maamuzi hivyo kupitia mafunzo haya yanawafanya kundi hilo kuongeza idadi ya viongozi na kufanana na kundi la wanaume katika nafasi za maamuzi.

Hata hivyo amesema amefurahishwa na ushiriki wa viongozi kutoka Zanzibar katika mafunzo hayo ambao mwaka huu wameitika kwa wingi ukilinganisha na mwaka uliopita.

''Jumla ya wahitimu 28 wamehitimu kozi za ngazi mbalimbali kwenye taasisi ya Uongozi kwa waliotoka Zanzibar hivyo hali hii inaridhisha sana,tutaendelea kutoa ruhusa ili viongozi wengi washiriki,''amesema.

Mhandisi Zainab Said pia amewashauri wahitimu wa kozi hizo wanaporudi katika maeneo yao ya kazi wakaoneshe tofauti kwa maneno na vitendo kutokana na mafunzo ambayo wameyapata kupitia kozi mbalimbali.

"Nendeni mkawe mabalozi wazuri, maana matendo yanu yatahamasisha wengine kujiunga na taasisi hii katika kusoma kozi mbalimbali za uongozi,"amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene akikabidhi vyeti kwa wahitimu kwenye mahafali ya Sita ya Taasisi ya uongozi ambapo wahitimu 196 wamehitimu kozi mbalimbali wakiwemo viongozi wanawake yaliyofanyika leo Mei 5,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
wahitimu 196 wa Taasisi ya Uongozi wakiwa kwenye Maandamano kwenye mahafali ya Sita ya Taasisi ya uongozi yaliyofanyika leo Mei 5,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene akizungumza kwenye mahafali ya Sita ya Taasisi ya uongozi ambapo wahitimu 196 wamehitimu kozi mbalimbali wakiwemo viongozi wanawake yaliyofanyika leo Mei 5,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo akizungumza kwenye mahafali ya Sita ya Taasisi ya uongozi ambapo wahitimu 196 wamehitimu kozi mbalimbali wakiwemo viongozi wanawake yaliyofanyika leo Mei 5,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zainab Said akizungumza kwenye mahafali ya Sita ya Taasisi ya uongozi ambapo wahitimu 196 wamehitimu kozi mbalimbali wakiwemo viongozi wanawake yaliyofanyika leo Mei 5,2023 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages