*****************
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetumia jukwaa la Maonesho ya Wiki ya Nishati 2023 kuwaeleza Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mpango uliopo na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau, Bw. Charles Nyangi, amesema tayari PURA imeanza maandalizi ya kufanya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia vilivyowazi kwa lengo la kuongeza uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa rasilimali hiyo nchini, uwekezaji ambao utawezesha ugunduzi zaidi wa gesi asilia au ugunduzi wa mafuta.
"Hivi sasa kazi zinazoendelea kama sehemu ya maandalizi ya kunadi vitalu ni pamoja na kudurusu Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato wa mwaka 2013 na kuainisha vitalu vitakavyonadiwa. Tukio la kunadi vitalu linatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka 2024" alieleza Bw. Nyangi.
Maonesho ya Wiki ya Nishati 2023 yameanza leo tarehe 29 Mei 2023 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 01, 2023. Maonesho hayo yanalenga kutoa uelewa zaidi kwa Waheshimiwa Wabunge kuhusu kazi na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake.