Breaking

Wednesday, 10 May 2023

ONGEZENI KASI UUNGANISHAJI HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI WA MIVUMONI- RC MAKALLA


Na Irene Thompson


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amefanya ziara ya kukagua hali ya upatikanaji  wa huduma ya maji kwa wananchi wa Mivumoni Wilaya ya Kinondoni baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa usambazaji maji wa Makongo hadi Bagamoyo uliogharimu zaidi ya Shilini bilioni 71 ambapo ametoa agizo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ya kuongeza kasi ya kuwaunganishia wananchi huduma hiyo.


Amesema hayo wakati akizungumza na wanachi wa Mivumoni kwenye mkutano wa hadhara baada ya kutembea nyumba kwa nyumba amewapongeza DAWASA kwa kazi nzuri inayoendelea ya kuunganisha maji kwa wakazi , Pia amesisitiza utoaji wa control number kwa wakati ili wananchi walipie huduma.


"Niwapongeze kwa kazi mnayoendelea kuifanya nimetembea kwenye mitaa kweli adhma ya Serikali ya kumtoa Mama kichwani inadhihirika, Ninasisitiza kasi ya kuunganisha wateja iongezeke na utoaji wa Control Number ufanyike kwa wakati" amesema Mhe. Makalla



Ziara hiyo imeenda sambamba na zoezi la utoaji wa vifaa kwa wananchi takribani 300 waliofika kwenye dawati la huduma kwa wateja ambapo ameridhishwa na juhudi za Mamlaka za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma kwa kuwaunganisha maji kwa mkopo.


Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa Mhe. Amos Makalla amekemea tabia ya urasimu kwenye kuwaunganisha wananchi ikiwemo kutoa huduma kwa upendeleo au kujuana.


Kwa niaba ya Kaimu Afisa Mtendaji Makuu Mhandisi Shabani Mkwanywe amesema mradi wa Makongo hadi Bagamoyo unategemea kunufaisha zaidi ya wateja 45,000 wa wilaya za Kinondoni, Ubungo na Bagamoyo, Kwa eneo la Mivoni wateja zaidi ya 15,000 wameunganishwa na huduma ya maji na zoezi bado linaendelea.


Pia, amewatoa hofu wakazi walio nje ya mita 50 kutoa eneo rasmi la mradi ya kuwa Mamlaka imeeandaa mpango mkakati wa usambazaji maji ambao utaenda kutatua changamoto iliyopo.


"Zaidi ya wakazi 2000 walibainika kuwa nje ya eneo rasmi la mradi hivyo kupelekea Mamlaka kuja na mpango rasmi wa kuhakikisha wanafikiwa na huduma ambapo hadi sasa wateja kati ya 655 wameunganishiwa huduma na zoezi la kuongeza mtandao umefanyika kwa umbali wa kilomita 16 kati ya kilomita 89 sawa na asilimia 18" amesema Mhandisi Mkwanywe


Mradi wa Usambazaji Maji Makongo hadi Bagamoyo ni maradi wa kimkakati unaotegemea kunufaisha maeneo ya Changanyikeni, Goba, Mivumoni, Mbweni, Madale, Bunju, Wazo, Ocean Bay, Salasala, Mapinga, Mabwepande, Mbopo, Kimara Ng'ombe, Ukuni, Mataya, Sanzale, Migude na Sehemu ya eneo la Mbezi

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages